Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa amewataka wananchi kushiriki katika vikao vya vijiji, kuchangia mawazo na kuibua miradi mbalimbali yenye manufaa kwao kwa kuwa Rais Samia amedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi wote wakiwemo wa hali ya chini.
Waziri Mchengerwa ametoa rai hiyo Disemba 17, 2021 alipofanya ziara na kukagua zahanati ya kijiji cha kakubilo iliyojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kwa asilimia 80 kwa kushirikiana na jamii ya kijiji cha kakubilo ambayo ilichangia kwa asilimia 20.
Amesema kuwa lengo la Rais Samia kuhusu Miradi hii ya TASAF ni kuzifikia kata milioni 1.5 katika vita vya kuondoa umasikini kwa kuboresha huduma za kijamii ili kumsaidia mtanzania mmoja moja katika mazingira yake.
Aidha ameendelea kusema kuwa viongozi wana jukumu la kuwasaidia wananchi kufikia ndoto zao za kimaendeleo kwa kuwatia moyo, kubeba fikra zao na kuzifanyia kazi ili kuwaboreshea miundombinu ya kufanyia shughuli zao kwa kuwa maendeleo ya Taifa hili yataletwa na Watanzania wenyewe.
Sanjari na hayo ametoa muda wa wiki mbili kwa watumishi wote wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuishi katika vituo vyao vya kazi badala ya Geita mjini ili kuwafikia na kuwahudumia wananchi kwa urahisi huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule kulisimamia hilo.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mratibu wa TASAF Halmashauri ya wilaya ya Geita Gabriel Evarist amesema kuwa Mradi huo wa zahanati unavisaidia vijiji vitano vya kata hiyo ya kakubilo huku akitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya huduma mbalimbali za kijamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa