Viongozi na watumishi wa Umma wametakiwa kutenga muda wa kusikiliza kero mbalimbali za watumishi wanaowaongoza katika maeneo yao kwa kuwa Serikali anataka kuona kila mtumishi akiwa na furaha sehemu yake ya kazi.
Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa ametoa wito huo Disemba 16 akiwa katika ukumbi wa GEDECO mkoani Geita alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Halmashauri za Wilaya, wakuu wa Taasisi za Serikali, na viongozi wa Mkoa.
Mchengerwa amesema kuwa endapo mtumishi atajengewa mazingira yenye kumpa furaha kazini itamuongezea kujiamini na kuzifanya kazi zake kwa ufanisi zaidi huku akiwataka viongozi mbalimbali na maafisa Utumishi kusikiliza kero za watumishi wanaowaongoza na kuzitafutia utatuzi badala ya kuwapuuza.
Aidha ameendelea kuwataka viongozi hao kutambua kuwa vyeo ni dhamana ya muda mfupi huku akiwasihi kutomfanyia mwananchi au mtumishi yeyote jambo ambalo yeye angefanyiwa jambo hilo asingelifurahia.
Sanjari na hayo amesisitiza kuwasilishwa mapema kwa taarifa za wastaafu miezi sita kabla katika ofisi za Utumishi makao makuu ili kuandaa mapema stahiki zao ili kuepuka usumbufu wa kufuatilia mafao kwa muda mrefu baada ya kustaafu huku akiwataka waajiri kutoa michango ya watumishi wao kwa wakati katika mifuko ya hifadhi.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mchengerwa Mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule alisema kuwa kwa kipindi cha kati ya mwezi Julai hadi Novemba mwaka huu Mkoa wa Geita umepokea kero 6,874 ambapo kero 5,442 zimepatiwa utatuzi huku kero 384 zikiendelea kutatuliwa ambapo kero nyingine zimewasilishwa ngazi za juu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa