Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Geita bibi Beatrice Munisi amewaasa wanaume nchini kuwasindikiza wenza wao kuhudhuria kliniki katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma kwa lengo la kujua maendeleo ya wenza wao na mtoto katika kipindi cha ujauzito.
Ameyasema hayo leo alipokua Akiongea na washiriki wa semina iliyoandaliwa na mradi wa USAID Boresha Afya unaofadhiliwa na shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID) wakati wa majadiliano ya kutengeneza mkataba wa utoaji wa huduma za afya kati ya Halmashauri na mteja iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Afisa wa Masuala ya Jinsia na vijana kutoka mradi wa boresha afya ndugu Revocatus Kadoshi akitoa ufafanuzi wa namna wauguzi na wakunga wanapaswa kutoa huduma bora kwa jamii
“Kumekuwa na tabia isiyopendeza kwa baadhi ya wanaume kutowasindikiza wenza wao kliniki na hii imepelekea migogoro mikubwa kwenye familia na wengi kutokufuatilia kabisa maendeleo ya mama na mtoto katika kipindi cha ujauzito na kujifungua. Ni wakati sasa wa wanaume kubadilika na kujua mtoto na mama wanahitaji uangalizi mkubwa katika kipindi hicho”. Amesema Munisi
Aidha kwa upande wa afisa wa masuala ya jinsia na vijana kutoka mradi wa USAID Boresha Afya bwana Revocatus Kadoshi amewaomba wauguzi na wakunga kutoa huduma za afya zenye utu, staha na kuzingatia heshima na haki za kijinsia kwa afya ya uzazi, mama wajawazito, watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano na huduma rafiki kwa vijana ili kuepuka migogoro na wateja wao.
Semina hiyo imeshirikisha wadau mbalimbali wa afya kutoka Halmashauri za Wilaya na Mji Geita kama vile waheshimiwa wenyeviti wa Halmashauri,wenyeviti wa kamati za kudumu za huduma za jamii, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, viongozi wa dini na wataalam mbalimbali kutoka halmashauri hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa