Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga, amewataka wananchi wanaopata huduma ya umeme kutumia nishati hiyo vizuri kwa maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogovidogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga akizungumza katika maonesho viwanja vya Bombambili
Wanga ametoa kauli hiyo akiwa katika viwanja vya Bombambili yanapofanyikia maonesho ya nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini, alipotembelea banda la Shirika la Umeme nchini TANESCO na kuelezwa namna Shirika hilo lilivyojipanga katika kuendelea kusambaza umeme vijijini.
Banda la Maonesho la Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Amewataka wananchi kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao mbalimbali yanayolimwa Geita,ili kuyauza maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Mkoa wa huu kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo kwa ujumla.
Kwa upande wake mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi.Furaha Paul Chiwile licha ya kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Geita, amesema kuwa Halmashauri hiyo imewawezesha wajasiriamali mbalimbali kwa kuwapatia mikopo, ambayo imewasaidia kufungua viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo ziko katika Banda hilo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi.Furaha Chiwile akionesha moja ya bidhaa zinazotengenezwa na Wajasiriamali wa Halmashauri hiyo.
Salome Chakupewa ni miongoni mwa Wajasiriamali ambao kupitia kikundi chao cha wanawake wa Igate wanaosindika mvinyo, anasema wamewezeshwa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 50 na Halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi jengo la kiwanda ambapo uzalishaji wa bidhaa zao unaendelea hadi sasa.
Bidhaa za mvinyo zinazotengenezwa na kikundi cha Wanawake wa Igate
Wakati huohuo Bi.Mwanahamis Said kutoka kikundi cha Mama ni Mama cha Nkome Mchangani wanaojihusisha na biashara ya dagaa, anasema kuwa licha ya kupatiwa mashine ya kukaushia dagaa kuwarahisishia shughuli zao lakini pia maonesho hayo ni fursa kubwa kwao kwa ajili ya kujitangaza wao na bidhaa zao.
Wanawake wa Nkome mchangani wakiwa na bidhaa zao za dagaa wanazozisindika
Maonesho hayo yameanza septemba 16 mwaka huu yakiratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambapo kilele chake ni septemba 26 na Mgeni Rasmi akiwa Waziri mkuu wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa anayetarajiwa kufika viwanjani hapo septemba 22,huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ’’SEKTA YA MADINI KWA UKUAJI WA UCHUMI NA MAENDELEO YA WATU”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa