Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya shilingi milioni 500 kwa vikundi 58 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hafla ya utoaji wa mikopo hiyo imefanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Geita tarehe Januari 5, 2026, ambapo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bi Janeth Mobe, alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Mhe Hashim Komba Mkuu wa Wilaya ya Geita.

Kaimu Mkuu wa Wilaya Bi Janeth Mobe akizungumza na wanavikundi waliojitokeza katika zoezi la ugawaji wa mikopo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw Jonas Kilave, amesema jumla ya vikundi 58 vimefanikiwa kupata mikopo hiyo baada ya kukidhi vigezo, kati ya vikundi vilivyokuwa vimewasilisha maombi ambavyo ni vikundi 94 vya wanawake, 92 vya vijana na 16 vya watu wenye ulemavu.
Ameongeza kuwa pamoja na utoaji wa mikopo, Halmashauri imeendelea kutoa mafunzo kwa wanufaika wa mikopo hiyo yakiwemo mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu za vikundi, usimamizi wa fedha, umuhimu wa kuweka akiba, ujasiriamali pamoja na utatuzi wa migogoro ndani ya vikundi.

Mkuu wa Divisheni ya maendeleo ya jamii Jonas Kilave akizungumza na wananchi waliojitokeza katika zoezi la ugawaji mikopo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Paschal Mapung’o, amevitaka vikundi vilivyopata mikopo hiyo kuitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija kwa jamii na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati.
Naye Mwakilishi wa TAKUKURU, Bw Said Lipunjaje, amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja ndani ya vikundi, akisema umoja huo uendelee hata baada ya kupokea mikopo ili malengo ya vikundi yafikiwe na marejesho yafanyike kwa wakati, hali itakayowawezesha wanufaika wengine kunufaika na mikopo hiyo.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Bi Leminatha Mbegete, amewataka wanufaika kuwa na nidhamu ya mikopo kwa kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati, akisisitiza kuwa mikopo hiyo iwe chachu ya maendeleo yao binafsi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Akihitimisha hafla hiyo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bi Janeth Mobe, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuandaa fedha kwa ajili ya vikundi, akisisitiza kuwa mikopo hiyo si hisani bali ni mikopo inayopaswa kurejeshwa kwa wakati. Ameongeza kuwa mikopo hiyo itumike vizuri ili iweze kusaidia vikundi vingine vingi zaidi siku zijazo. Aidha amewaasa wanufaika kuwa mabalozi wazuri wa serikali kwa kuitangaza na kuonesha jitihada zake za kuwajali wananchi. Kwa upande wa waendesha bodaboda, amesisitiza umuhimu wa kuwa na leseni halali.

Kaimu Mkuu wa Wilaya Bi Janeth Mobe akikata utepe kurasmisha zoezi la utoaji mikopo kwa vikundi
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Jumanne Misungwi, amesema serikali ipo pamoja na wananchi na inaendelea kuwatambua, huku akisisitiza suala la uzalendo kwa vijana. Amewataka wazazi na walezi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwalea na kuwaelimisha vijana katika misingi ya uzalendo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Jumanne Misungwi akizungumza na wananchi waliojitokeza katika zoezi la ugawaji wa mikopo kwa vikundi
Kwa upande wa wanufaika, Bi Furaha Yusufu mkazi wa Katoro na mwakilishi wa vikundi vya vijana, amesema mikopo hiyo itamsaidia kuendeleza biashara ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kama viatu na hivyo kuboresha maisha yake na kuwa mlipa kodi mzuri.
Naye Mwakilishi wa wanawake, Mama Sabina Kaitila kutoka Tarafa ya Bugando na Mwenyekiti wa Kikundi cha Kazabuti, ameishukuru serikali kwa kutoa mikopo hiyo akisema itawasaidia wanawake wengi kujiimarisha kiuchumi na kuepuka changamoto zilizokuwa zikisababishwa na mikopo isiyo rafiki.
Kwa upande wake, Bw Hamisi Masegenya, Mwenyekiti wa Kikundi cha Abhabhelu, ameishukuru serikali na kuomba siku zijazo wapewe vyombo vya moto ili waweze kuongeza kipato chao.
Mikopo hiyo ni sehemu ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayotengwa kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.



Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu wakiwa wameshika mfano wa hundi ya Sh Milioni 500 wakati wa upokeaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa