Programu ya Mradi wa Elimu unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya nchini Korea, (KNC-UNESCO), Bridge-Tanzania, leo Januari 7, 2025, umezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Mradi huo umewalenga vijana kwa kuwapatia stadi mbalimbali pamoja na ujuzi ili waweze kujiongezea tija kwenye shughuli zao ka kuchangia pato la familia, jamii, na taifa kwa ujumla.

Ukiwa umetambulishwa toka mwaka 2024, mradi huo una lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na vijana takribani 1,050 kutoka kata 10 pamoja na kuwafaidisha na utaendeshwa kwa awamu tano.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Ofisi za Kata, Nzera, Katibu Mtendaji kutoka tume hiyo, Prof. Hamisi Masanja Malebo amesema kuwa dhumuni la mradi huo ni kuwavusha vijana kuelekea ajenda ya dunia ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 huku akiwataka washiriki wa programu hiyo kuweka nia na juhudi ili malengo ya mradi huo yawe yenye matokeo chanya kwenye jamii.
Prof. Malebo ameongeza kuwa, maono ya Bridge - Tanzania yanaendana na maono ya Mhe. Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa kuwekeza kwenye Elimu jumuishi na ujenzi wa uwezo wa vijana. Alifafanua kuwa, kupitia dira hiyo, Serikali inalenga kuhakikisha vijana wanapata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Ndg. Jonas Kilave amewataka vijana hao kuonyesha nidhamu ya kujifunza na kuufanyia kazi ujuzi watakaoupata. Ameongeza kwa kutoa wito kwa vijana hao kuunda vikundi ili waweze kunufaika na fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali pamoja na kuwatumia wataalamu kwenye kuanzisha miradi ya kimaendeleo.


Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa