Mkuu wa wilaya ya Geita Mh Wilson Samwel Shimo amewatoa hofu wanafunzi wa shule ya Sekondari Lwezera, kufuatia ajali ya radi iliyotokea leo Agosti11, 2021 na kuwajeruhi wanafunzi 16 wa shule hiyo.
Ajali hiyo ya radi imetokea leo majira ya saa tano asubuhi wakati wanafunzi wakiwa wanaendelea na ratiba zao za masomo ambapo wanafunzi wanane ni wasichana na wanane wengine ni wavulana huku kati ya hao wasichana watatu na wavulana wawili wamelazwa katika Hospitali ya wilaya Nzera.
Tukio la ajali hiyo ya radi limetokea wakati ambapo Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Geita Wilson shimo akiwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita na kulazimika kuacha kikao hicho na kuelekea eneo la tukio.
Akiwa katika shule ya Lwezera ilipotokea ajali hiyo Mh Wilson Shimo amezungumza na uongozi wa shule na wanafunzi ambapo amewataka wanafunzi kuwa watulivu na kuendelea na masomo kama kawaidia na kuagiza ukaguzi ufanyike kubaini vitu vinavyoweza kuvuta radi katika shule hiyo ili kujihadhari.
Aidha Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dr. Modest Rwekaemula, amesema walipopata taarifa hizo hatua ya kwanza walipofika shuleni hapo waliwachukua wanafunzi wote waliopata madhara na kuwakimbiza katika zahanati ya Lwezera ambapo baadhi wamepewa huduma ya kwanza na wengine kulazimika kuwapeleka Hospitali ya wilaya nzera kwa ajili ya matibabu zaidi.
Amesema kwamba wamepatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri na kuongeza kuwa wameshatoa elimu kila shule namna ya kuchukua tahadhari na kukabiliana na majanga kama hayo ikiwemo kutoa taarifa katika zahanati iliyo karibu na kutoa taarifa katika uongozi wa wilaya ili kuongeza nguvu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lwezera Mh. Misango Jeremiah Misango amewasihi wanafunzi wasiwe na hofu bali waendelee na masomo wakiamini kuwa Serikali inawatambua na kuwajali.
Hata hivyo baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo akiwemo Anastazia Richard na Veneranda Myengi wamesema wakiwa darasani gafla ilipiga radi iliyowafanya wapoteze fahamu kwa mshtuko na baadae kujikuta wakiwa Hospitalini wakiwa na maumivu makali mwilini.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa