Na: Hendrick Msangi
Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inajukumu la kukusanya takwimu za Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.
Takwimu hizo hukusanywa kila Mwaka kama zinavyokuwa tarehe 31Mwezi Machi kwa kutumia Madodoso ya Takwimu za shule/madarasa ya Elimu ya Awali (TSA), Takwimu za Shule za Msingi (TSM), Takwimu za Elimu ya Sekondari (TSS) naTakwimuza Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (TWM).
Lengo la kukusanya takwimu hizi ni kutoa taarifa na picha ya hali halisi iliyofikiwa kutokana na viashiria mbalimbali vya kielimu katika Sekta ya Elimu msingi, Elimu ya Sekondari Kidato cha Tano na Sita na Elimu ya Watu Wazima. Viashiria hivyo huonesha ni kwa kiasi gani utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo umefanikiwa.
Ili kufikia lengo la kukusanya taarifa hizo muhimu kwa usahihi, Mwongozo huo umeandaliwa kuwezesha wanaohusika na ukusanyaji wa taarifa hizo kuelewa kwa ufasaha maswali na takwimu zinazohitajika katika kufanikisha zoezi lengwa.
Wakuu wa shule za Msingi na Maafisa Elimu kata wakiwa kwenye semina elekezi ya ukusanyaji wa Takwimu sahihi Halmashauri ya wilaya ya Geita. Zoezi hilo linatarajiwa kuhitimishwa na Afisa Elimu wa Halmashauri kwa kufanya Uhakiki na kuthibitisha (Approve) Usahihi wa takwimu katika mfumo kwa kila Shule kabla ya tarehe 8 Mei, 2024.
Katika kutekeleza hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imefanya kikao kazi na walimu wakuu wa shule zote za msingi, maafisa elimu kata na walimu wenye dhamana ya kutunza takwimu kwenye shule za msingi ili kuendelea kuwajengea uwezo wa kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa Taifa.
Akifungua semina hiyo elekezi, Kaimu Mkuu wa Idara ya elimu ya awali na msingi Mwl Richard Paul Magubiki alisema zoezi la takwimu linafanyika kila mwaka na lina maana kubwa sana katika shughuli zote za kiserikali kama ilivyo Sheria ya Takwimu Na.9 ya Mwaka 2015 inavyosisitiza utoaiji wa takwimu zilizo sahihi “Takwimu ndio kiini cha kila kitu hivyo kila mtu ahakikishe anatoa takwimu zilizo sahihi kwani kutokutoa takwimu zisizo sahihi kunaiingizia serikali hasara kubwa” alisema Mwl Magubiki.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu ya awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mwl Magubiki akiwa na maafisa Elimu wa Halmashauri katika semina elekezi kwa wakuu wa shule ,walimu wa takwimu na maafisa elimu kata ya ujazaji wa takwimu sahihi
Akiendelea kuwapa semina elekezi walimu hao, Mwl Magubiki alisema Takwimu husaidia kubaini mahitaji muhimu katika sekta ya elimu, kujua kuna nini katika elimu ya msingi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya thamani zilizopo,idadi ya wananafunzi, walimu na kufahamu mapungufu katika sekta ya elimu.
Aidha Mwl Magubiki alisema zoezi hilo likifanywa kwa ukamilifu litasaidia serikali kupanga bajeti kwa kutumia takwimu zilizo sahihi na kuwataka walimu hao na watakwimu kutojifungia mashuleni bali kushirikiana kupata taarifa sahihi kwa kujipanga mapema ili zoezi hilo likamilike kwa wakati na kuleta matokeo chanya yenye uhalisia.
Wakuu wa Shule, Walimu wa Takwimu na Maafisa Elimu Kata kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita walipokutana katika kikao elekezi kutekeleza Sheria ya Takwimu Na.9 ya Mwaka 2015 ambayo ni miongoni mwa Sheria zilizofanyiwa urekebu (revision) Mwaka 2019 na kutangazwa na Serikali tarehe 28 Februari, 2020 (GN 140/2020). Urekebu huo katika Sheria ya Takwimu unajumuisha marekesho ya Mwaka 2018 na 2019.Kwa mantiki hiyo, kuanzia tarehe 28 Februari, 2020, Sheria ya Takwimu itanukuliwa kama “Sheria ya Takwimu, SURA 351
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina jumla ya shule za msingi 246 za serikali zikiwa 235 na shule binafsi 11 na walimu 3258. Zoezi la Uhakiki na kuthibitisha (Approve) Usahihi wa takwimu katika mfumo kwa kila Shule linatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 8 Mei, 2024.
Maafisa Elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa kwenye kikao na wakuu wa shule, maafisa elimu kata na walimu wa takwimu katika semina elekezi iliyofanyika shule ya msingi Nzera.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa