Katika jitihada za kutatua changamoto ya uhaba wa madawati katika shule mbalimbali za msingi, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeamua kutumia mapato yake ya ndani kugharamia ununuzi wa madawati hayo.

Akizungumza katika hafla ya kugawa madawati zaidi ya 600 kwa shule za Halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza menejimenti ya Halmashauri na Baraza la Madiwani kwa uamuzi wao wa kutenga fedha za ndani kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo inayowakumba wanafunzi na walimu.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ibrahim Bunangoi, amesema wamepokea kwa mikono miwili maelekezo ya Mkuu wa Wilaya katika kuhakikisha suala la uhaba wa madawati linafanyiwa kazi.
Baadhi ya walimu waliopokea madawati hayo wamesema wanashukuru kwa msaada huo na kuipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kutatua changamoto hiyo.Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina jumla ya shule za msingi 238, zenye wanafunzi 258,318.

Hata hivyo, madawati yaliyotolewa ni 677, ambayo yanaweza kutumika na wanafunzi 2,031. Hii ina maana kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa madawati katika shule nyingi za wilaya hiyo.
Hivyo, wadau wa elimu wanashauriwa kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuondoa changamoto hii na kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata fursa ya kujifunza katika mazingira bora.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa