Wajumbe wa mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi - CCM Wilaya ya Geita leo februari 19, mwaka 2022 wameridhishwa na namna viongozi wa serikali wanavyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 katika Wilaya ya Geita.
Mkutano huo umefayika katika ukumbi wa GEDECO mjini Geita kwa kuongozwa na mwenyekiti wake Barnabas Mapande ambapo pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umepokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM kuanzi mwezi Julai hadi Disemba mwaka 2021 kutoka katika Halmashauri za Wilaya na mji Geita, TANESCO, TARURA, RUWASA na GEUWASA.
Mkutano huo umeazimia kwa kauli moja kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hasan kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na kuahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu 2022.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba Mwaka 2021, Halmashauri imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 7.2 ambayo ni sawa na asilimia 47.8 na kwamba mapato ya ndani ni shilingi bilioni 2.4 sawa na asilimia 53.
Mkurugenzi John Paul Wanga amesema katika sekta ya Afya katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2021, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetekeleza shughuli za upauaji wa majengo 12 ya OPD kwa gharama ya shilingi milioni mia moja sitini na tatu mia nne themanini na mbili elfu na mia nane arobaini.
Wakati huohuo ukamilishaji wa jengo la wagonjwa wa nje umegharimu kiasi cha shilingi milioni thelathini na mbili mia nne themanini na tatu elfu mia nne ishirini na saba, huku ujenzi wa nyumba sita za watumishi (TWO IN ONE) ukigharimu kiasi cha shilingi milioni themanini na nne mia nne na nane elfu na mia sita.
Aidha sekta ya afya pia imepokea shilingi milioni mia mbili kwa ajili ya kukamilisha zahanati nne katika kata za Lubanga, Busanda, Nyamboge na Nyang’hanga ambapo ujenzi wa miradi hiyo upo katika hatua za ukamilishaji.
Mkurugenzi John Paul Wanga ameueleza mkutano huo wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita kwamba kupitia mapato ya ndani Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa shilingi milioni mia moja tisini kukamilisha miundombinu ya sekta ya Afya.
Aidha kupitia mapato ya ndani pia Halmashauri inajenga kituo cha Afya kwa shilingi milioni 500 katika kijiji cha Ibisabageni kwa kuanza na majengo ya vipaumbele kama vile jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, jengo la ufuaji, wodi ya wazazi na upasuaji na jengo la kuhifadhia mahiti.
Pia Halmashauri ilipokea fedha za tozo shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na maabara katika kituo cha Afya cha Bugalama.
Katika idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri imetoa jumla ya shiligi milioni 180 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo mikopo hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani vikundi vimeanzisha miradi kwa ajili ya kujiongezea kipato na kuzalisha ajira.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Geita Bi. Alexandrina Katabi ameimwagiwa sifa Halmashauri ya wilaya ya Geita kwa kufanya vizuri katika kutenga fedha asilimia 10% kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu na kuwataka kuendelea hivyo huku akiishauri Halmashauri ya wilaya ya Geita kwamba pesa zinazotolewa ziwe za uhakika ili kikundi kitakachopata fedha hizo kiweze kufanya kazi vizuri zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa