Wananchi Wilayani Geita wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo pamoja na wajasijiriamali wametakiwa kuhakikisha wanazikatia biashara zao leseni pamoja na kuwa na vibali halali kutoka serikalini ili kuweza kufanya biashara zao kwa uhakika na kuepukana na adha wanayoweza kukumbana nayo ya kufungiwa biashara hizo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao wa Kata za Nkome, Nyamboge, Lwezera na Nzera katika zoezi la uelimishaji na ukaguzi wa vibali na leseni halali za biashara, Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bw. Dennis John Lihepa amewataka wafanyabiashara hao kuondokana na tabia ya kufanya biashara kiholela bila ya kuwa na leseni na vibali stahiki, kwani kufanya hivyo ni kuikosesha serikali mapato ambayo ni msingi wa maendeleo kwa kuchangia miradi mbalimbali katika jamii.
Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bw. Dennis John Lihepa akiwa katika zoezi la uelimishaji na utoaji wa leseni za biashara kwa baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka ya jumla na wasimamizi wa nyumba za kulala wageni kwenye Kata ya Nkome.
“Kama mfanyabiashara, unapaswa kuhakikisha unaikatia biashara yako leseni, pamoja na kuwa na vibali stahiki vitakavyowezesha kufanya biashara yako kwa amani na utulivu. Lakini pia unapaswa kutambua kuwa, kwa kuikatia leseni bishara yako, unakuwa umechangia katika kuleta maendeleo kwenye jamii kwani fedha inayopatikana ndiyo inayowezesha utekelezaji wa miradi mbali mbali kwenye Halmashauri.” Amesema Bw. Lihepa.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara waliotembelewa na timu hiyo, wameipongeza Serikali kwa hatua hiyo, huku wakiitaka elimu hiyo kwa mfanyabiashara kutolewa mara kwa mara ili kuwawezesha wafanyabiashara kuwa na uelewa zaidi wa masuala ya kodi.
Baadhi ya maduka katika Kata ya Nkome yaliyofikiwa na huduma ya urasimishwaji wa biashara kwa kukatiwa leseni na Maafisa Biashara kutoka Halmashauri.
“Kwa hakika hatua hii ni ya kupongezwa kwa serikali kwasababu inatuwezesha sisi kama wafanyabiashara kutambua nini tunapaswa kufanya ili kuzirasimisha biashara zetu. Tunapenda kutoa wito kwa Serikiali kuhakikisha inatoa elimu hii kwa wafanyabiashara mara kwa mara ili kuwapa uelewa wa faida za kulipa kodi na namna tunavyoweza kuchangia katika kuleta maendeleo kwenye jamii yetu.” Amesema Bi. Sophia Ngoni anaejishughulisha na biashara ya saluni.
Zoezi la utoaji elimu kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipia leseni za biashara ni endelevu katika kuhakikisha Halmashauri inafikia malengo yake katika ukusanyaji wa Mapato ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 Halmashauri kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato inatarajia kukusanya zaidi ya Bilioni 8.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa