Baada ya kukutana na Wadau mbalimbali wa Elimu kuanzia ngazi za Vijiji, na Kata, Shirika la Plan International June 02, 2022 lilikutana na Wadau wa Elimu ngazi ya Halmashauri katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera, kwa lengo la kujadili changamoto, maendeleo na kuweka mikakati ya kuendelea kumlinda Mtoto.
Kwa mujibu wa Ndg. Abeid Mkwawa Mratibu wa Mradi wa kutokomeza ajira kwa watoto mkoa wa Geita, Halmashauri ya Wilaya Geita imefanikiwa katika mambo mbalimbali yanayomhusu mtoto ikiwemo huduma ya Chakula mashuleni, upatikanaji wa huduma ya maji na vyumba maalumu vya hedhi salama mashuleni, usalama wa watoto na kukomesha ajira za watoto hasa katika maeneo ya shughuli za uvuvi na uchimbaji wa madini.
Miongoni mwa mbinu zinazotajwa na Ndg. Mkwawa kutumika katika kufanikisha hali hizo ni pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali kwa kuwapatia Elimu ya Haki za watoto zinazopaswa kulindwa sambamba na kuunda kamati mbalimbali kuanzia ngazi za Shule, Vijiji na Kata ambazo zimekuwa zikifuatilia na kuchukua hatua kwa kuwasaidia watoto hao ikiwemo kuwarudisha mashuleni watoto wanaojiingiza katika shughuli za uzalishaji mali.
Wadau wanaziona changamoto mbalimbali kama vile lishe duni kwa watoto, mazingira yasiyo vutivu ya kujifunzia, huduma za maji na vyumba vya hedhi salama mashuleni kuchangia kudhorotesha maendeleo ya kitaaluma na ufaulu wa watoto huku wakiweka mikakati mbalimbali ya kuendelea kuboresha hali za wanafunzi mashuleni.
Wadau wameazimia kutoa Elimu na hamasa kwa wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali ili wafahamu umuhimu wa chakula mashuleni na miundombinu rafiki ya Hedhi salama, suala litakalowafanya kuhamasika kuchangia maendeleo ya hali hizo ili kumsaidia mtoto kusoma katika mazingira salama na kuongeza ufaulu kwa ujumla.
Aidha wadau wameshauri pia kutumia mashamba ya shule na vipindi vya Elimu ya Kujitegemea (EK) kwa ajili ya kuzalisha chakula cha wanafunzi shuleni huku wakiwashirikisha wataalamu wa kilimo ambao watashauri kitaalamu kuhusu mazao yanayotakiwa kuzalishwa katika maeneo husika kulingana na hali za mashamba hayo.
Shirika la Kivulini linaloshirikana na PLAN limefanikiwa kuwatumia wataalamu wa huduma za Afya kufundisha jinsi ya kutengeneza Sodo kwa ajili ya wanafunzi wa kike mashuleni huku ujuzi huo ukiendelea kutolewa kwa jamii ili kuwasaidia kupunguza gharama za kununua taulo za kike ambazo wanafunzi wengine wanashindwa kugharamia.
Katika kuona unyeti wa changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina mkakati wa kutenga chumba maalumu cha hedhi salama katika majengo ya vyoo yanayojengwa kwa sasa ili kupunguza changamoto hiyo ambapo pia wadau wanaomba kuwepo kwa madawati ya jinsia angalau katika kila kata ili kuongeza ufuatiliaji wa kesi za ukatili dhidi ya watoto.
Ufinyu wa bajeti unatajwa kutotosheleza mahitaji ya walengwa suala ambalo wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali wana wajibu wa kusaidia katika kutatua changamoto hizo ili kuepuka kumnyanyasa mtoto kwa kujua au kutokujua ingawa uwepo wa fedha za kutosha ungeweza kusaidia hata kununua vifaa ambavyo vingeweza kutumiwa na wanafunzi wenyewe kutengeneza Sodo ambazo wangezitumia wakiwa shuleni kuliko kuacha kuhudhuria masomo.
Aidha jamii pia inawajibika kuwahudumia watoto kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ya msingi ikiwemo huduma za Afya, Chakula na malazi na kutotimiza wajibu huo ni kumnyanyasa mtoto.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa