Katika jitihada za kuimarisha usalama kuelekea uchaguzi mkuu, viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya katika Mkoa wa Geita walihudhuria mafunzo elekezi yaliyofanyika tarehe 4 Aprili 2025. Mafunzo hayo yalilenga kuongeza ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kupambana na uhalifu.
Kamishna Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Safia Jongo, alibainisha kuwa matukio makubwa ya uhalifu, kama vile mauaji na watu kushindwa kutembea usiku, yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana ili kuimarisha usalama, hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dkt. Modest Burchad, alieleza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kudumisha amani na usalama katika mkoa huo. Alipongeza juhudi za Jeshi la Polisi katika kupunguza uhalifu na kuleta matokeo chanya yanayoonekana.
Katika mafunzo hayo, Kamishna wa Polisi, F.C. Shilogile, alieleza faida za ulinzi shirikishi, ikiwemo kuimarisha usalama kupitia taarifa kutoka kwa wananchi, kujenga mahusiano bora kati ya polisi na jamii, na kupunguza vitendo vya uhalifu. Alisisitiza kuwa polisi ni sehemu ya jamii na wanapaswa kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kufanikisha malengo ya pamoja ya usalama.
Aidha, ilielezwa kuwa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) inafadhili vikundi mbalimbali vya vijana 982 katika kata na vijiji vya mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama na maendeleo ya jamii. Mafunzo hayo pia yalijumuisha mada kuhusu nafasi ya viongozi katika ushirikishwaji wa jamii na ulinzi shirikishi, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto, pamoja na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii, hivyo kusaidia katika kudumisha amani na usalama katika Mkoa wa Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa