Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024, Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava amewataka vijana kuishi yale waliyoelezwa kwenye kongamano ili kuwa na mchango chanya kwenye jamii zao pamoja na kuepukana na tabia hatarishi ili waweze kuyafikia malengo yao.
Akizungumza na Vijana wa kata ya Nkome Wilayani Geita, Ndg. Godfrey Mnzava amesema kuwa vijana wanapaswa kuzinoa fikra zao ili ziwe na tija kwenye taifa pamoja na kuwa wazalendo.
"Vijana wanatakiwa watekeleze yale yaliyosemwa kwenye kongamano hili la vijana ili kuendelea kuzinoa fikra zao ziwe zenye kuleta matokeo makubwa na hivyo kuleta faida kwa jamii na taifa kwa ujumla." Amesema Ndg. Mnzava.
Vijana Wilayani Geita wametakiwa kuyafanyia kazi yale waliyoelezwa kwenye kongamano ili kuwa na mchango kwenye jamii.
Aidha, kiongozi huyo pia amewataka waratibu wa kongamano hizo kuhakikisha wanakuwa na vikao vya mara kwa mara na vijana ili kuwa na mchango kwenye jamii.
"Tuendelee kuzungumza na vijana mara kwa mara, ikiwezekana mara nne kwa mwaka tukiendelea kuwatengeneza kwa kuwa ni nguvu kazi ya taifa. Hii itasaidia hata wao kuziangalia fursa kwa mtazamo wa kipekee, lakini pia itawapa nafasi vijana kutoa maoni yao."
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bi. Mathalena Mgina, amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo inyotolewa na Halmashauri ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
"Jukumu letu sisi kama Halmashauri ni kuhakikisha tunawasaidia kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na suala la utegemezi kwenye jamii yetu. Ili kuweza kupata mikopo ambayo inatolewa na Halmashauri, mnapaswa kuanzisha au kujiunga kwenye vikundi ili muweze kufaidika na mikopo hii." Amesema Bi. Mathalena.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bi. Mathalena Mgina, amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Mada zilizofundishwa kwa vijana ni pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika Halmashauri ya Wilaya, VETA, SIDO Pamoja na Benki ya NBC huku vijana wakiitaka serikali kuendelea kupewa mikopo isiyo na riba kwa wakati, kujengewa uwezo kwenye masuala mtambuka, pamoja na kushirikishwa kwenye vyombo vya maamuzi.
Meneja Benki Ndugu Amiri Mhina kutoka Benki ya NBC Geita amewasisistiza vijana kuwa na tabia ya kujiwekea akiba kwaajili ya badae.
Elimu ya Uzalendo na Uadilifu iliwasilishwa na Ndugu Ally Ally Abdul Mkurugenzi Chuo Kikuu Huria Tanzania Geita aliyewaasa vijana kuwa wazalendo, wajiamini, Pamoja na kuwa waadilifu.
Bakari Moshi Kitoboli (Afisa Uendelezaji Biashara) kutoka SIDO Geita amewataka vijana kuwa na dhana ya kujitegemea kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo zinazoweza kuwaingizia kipato.
Mganga Mfawidhi kutoka Zahanati ya Nkome, Dkt. Charles Kafulela amewataka vijana kutambua changamoto zinazowakabili kwenye mazingira yao na kuzigeuza kuwa fursa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa