Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia umefanyika leo Januari 26,2025 Mkoani Geita.
Akimuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe Dotto Mashaka Biteko( MB), Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela amezindua Kampeni hiyo ambayo Wizara ya Katiba na Sheria imekasimiwa kuratibu Kampeni hiyo.
Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Kalangalala ambapo Taasisi mbalimbali zimehudhuria ambazo ni wakala wa usajili ufilisi na udhamini(RITA), Tanganyika Law Society (TLS) na Shirika la NELICO.
Mhe Shigela amesema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan inatambua wananchi wengi wanakosa msaada wa kisheria kwa kuwa gharama za kulipa Mawakili ni kubwa.
"Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ameona wapo watanzania ambao hawana uwezo wa kulipa Mawakili ili kupata huduma za kisheria hivyo Serikali inayofedha ya kuwalipa Mawakili ili wananchi wanufaike na huduma ya msaada wa kisheria" Amesema Mhe Shigela.
Aidha Mhe Shigela amesema Kampeni hiyo inaongeza wigo wa kupata elimu na kupata huduma za kisheria ikiwa ni pamoja na kupanua utawala bora na demokrasi na kupunguza matatizo ambayo yanahitaji msaada wa kisheria Bila kujali umri na uwezo wa wananchi.
"Tuendelee kujipanga na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili mambo yanayowakabili wananchi hasa kwenye madini, ardhi, Mirathi , ndoa, ukatili wa kijinsia na watoto yaweze kupatiwa ufumbuzi na yale mambo yatakayobainika na kupelekwa mahakamani basi wananchi wajitokeze kwenda kutoa ushahidi. " Ameongeza Mhe Shigela.
"Mjitokeze kutoa ushahidi kwani Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan anazo fedha za kuwalipa mawakili wote wanaosimamia hizo kesi. Tujipange kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma" Amesisitiza Mhe Shigela.
Pamoja na hayo Mhe Martine Shigela ametoa wito kwa wananchi waliohudhuria uzinduzi huo kuwa Mabalozi kwa wengine ili waweze kujitokeza kupata huduma hiyo. Vilevile Mhe Shigela amezitaka Taasisi mbalimbali, vyama vya siasa, Taasisi za Kidini Pamoja na vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa na kuhamasisha wananchi ili kujitokeza katika kampeni hiyo.
"Niwasihi kujipanga kuhamasisha wananchi, Viongozi wa Dini hii iwe sehemu ya Ibada kwani wananchi wanapopata huduma mnapata thawabu" Ameongeza Mhe Shigela.
Akihitimisha hotuba yake Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema dhamira ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuwahudumia Watanzania na ameendelea kuwa na ubunifu kila wakati kuigusa mioyo ya watu waliopoteza haki zao na kutoa wito kwa Mawakili wanaosimamia mashauri ya wananchi kuyapeleka mahakamani yale yanayotakiwa huku akiwasihi wananchi kujitokeza kutoa ushahidi wanapohitajika.
Mkoa wa Geita una jumla ya Halmashauri Sita ambazo kila Halmashauri inatarajiwa kufikiwa kwa idadi ya kata 10.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa