Viongozi wa baraza la wazee waliochaguliwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wametakiwa kutambua na kuwajibika ipasavyo kwa majukumu ya baraza wakishirikiana na Mratibu wa wazee wa Halmashauri hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya Thomas Dimme aliyasema hayo wakati akijibu risala ya wazee wa baraza, akiwa ni mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Geita ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa baraza la wazee wa Halmashauri.
Dimme amesema endapo viongozi hao watawajibika kufanya majukumu yao changamoto zinazowakabili wazee kiuchumi, kiafya na kijamii zitapungua.
“Viongozi wa baraza mliochaguliwa mnawajibu wa Kutetea masuala ya wazee kwa Serikali, mashirika ya umma na wadau mbalimbali, kuhakikisha Baraza la Wazee linakaa kila robo kwa mujibu wa sera, pamoja na kuhakikisha huduma katika madirisha ya wazee katika vituo vyote vya afya zinazingatiwa ipasavyo pamoja na mengineyo”,amesema Dimme.
Hata hivyo Dimme amewapongeza wajumbe wa kikao hicho muhimu kitakachosimamia ustawi, maslahi pamoja na maendeleo ya wazee ndani ya Halmashauri.
Kwa upande wao viongozi waliochaguliwa waliomba ushirikiano kutoka kwa wajumbe wote ili kuwezesha baraza kufikia malengo yake, kubwa ikiwa ni kuwapatia Ustawi na Maendeleo Wazee wote ndani ya Halmashauri.
Hata hivyo kikao hicho kimeweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za wazee baadhi ikiwa ni; kusimamia mabaraza ya wazee ngazi zote za Halmashauri, Kata na Vijiji, kukutana angalau kila robo kutathimini hali ya ustawi wa wazee katika ngazi husika na kuhuisha takwimu za wazee katika Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa