Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (UNESCO-NATCOM) imeendesha mafunzo ya programu maalumu ya kuboresha uhifadhi kilimo na uchakataji wa Mimea-Dawa pamoja na tiba lishe kwa Wataalamu wa Tiba Asili Halmashauri ya Wilaya ya Geita, huku lengo likiwa ni kupanua wigo wa huduma ya afya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo ya Awamu ya kwanza tarehe 1, Julai na Wataalamu wa Tiba Asili kutoka Vijiji vya Nungwe na Mharamba, Mshauri wa ndani wa masuala ya Afya kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dkt. Rogers Mwakalukwa amesema kuwa, dawa za asili zina mchango mkubwa kwenye sekta ya afya ambapo takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya 60% ya wananchi wanatumia dawa za asili huku zaidi ya 50% ya dawa zote zinatokana na mimea.
Aidha, Dkt. Rogers pia amesema Sera ya Taifa ya Afya, Sheria Na. 23 ya mwaka 2002 inatambua huduma za tiba asili kama mojawapo ya huduma rasmi za afya nchini, na kwamba kanuni, miongozo na taratibu pia zipo, na hivyo kuwataka wataalamu hao wahakikishe wanajisajili kupitia Mfumo wa Rufaa (Enhanced Referral System) ili waweze kutambulika rasmi pamoja na kushirikiana na Hospitali na Vituo vya Afya wilayani humo.
Kwa upande mwingine, Mtaalamu wa Mimea, Bw. Frank Mbago amesema kuwa, mchango mkubwa wa afya ya binadamu unatokana na mimea, hivyo Wataalamu wa Tiba Asili wanapaswa kuchukua hatua kuhakikisha wanaitunza na kuiendeleza mimea hiyo ili iweze kuleta manufaa kwenye jamii.
Bw. Mbago pia amewasisitiza wataalamu hao kurithisha utaalamu unaotokana na Tiba Asili kwa vizazi vijavyo ili huduma hiyo iwe endelevu na kuangalia namna bora ya kuitunza na kuitumia mimea asili kama dawa.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya, Geita, Bi. Beatrice Munisi amesema kuwa Serikali imeanzisha utaratibu wa kuhakikisha uratibu wa huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala zinapatikana katika ngazi zote za Mkoa na Halmashauri ili kuwapa unafuu Wataalamu wa Tiba Asili kufanya shughuli zao.
Bi. Beatrice pia ametoa wito kwa wataalamu hao kushirikiana na watoa huduma za Tiba za Kisasa kwa lengo la kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kudumisha huduma zinazozingatia usalama na ufanisi wa huduma za afya wilayani humo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa