Kiitikio cha salamu mpya hapa nchini Tanzania kijulikanacho kama “kazi iendelee” kimeendelea kudhihirika mkoani Geita Aprili 17, 2021 baada ya mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel kuweka mawe ya msingi katika shule za sekondari mpya tatu za Izumacheli, Mnyala pamoja na Katoma kati ya zinazoendelea kujengwa ndani ya halmashauri ya wilaya ya Geita, jimbo la Geita ikiwa ni jimbo la sita kutembelewa katika ziara yake kuyatembelea majimbo saba ya mkoa mzima.
Katika ziara yake, mhandisi Gabriel ameeleza kufurahishwa kwake kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa kwenye shule hizo na kuahidi kuwa, kwaiba ya serikali atahakikisha anaendelea kuunga mkono jitihada zilizooneshwa na wananchi, wadau pamoja na halmashauri katika kuongeza miundombinu ili kuwasaidia wanafunzi ndani ya kata zao, huku akiwakumbusha wadau mbalimbali wa maendeleo ndani ya Geita kuikumbuka kata ya Izumacheli ambayo ipo ndani ya kisiwa lakini pia kuutaka uongozi kuweka jitihada kumalizia madarasa yaliyobaki na kuanza ujenzi wa mabweni pamoja na maabara.
“hii ni ziara yangu kwa mkoa mzima, nimefarijika sana kwa jinsi mnavyojituma kufanya kazi. Pongezi kwenu kampuni za African Underground Mining Services ltd, AKO Group Ltd, Eagle Brand Mining ltd, na Capital Drilling bila kumsahau mbunge Joseph Musukuma kwa kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi katika kujiletea maendeleo, hivyo na makampuni mengine Geita muikumbuke Izumacheli na shule nyingine pia” alisema mhandisi Gabriel.
Akihitimisha ziara yake, mhandisi Gabriel amewataka wazazi wawahimize watoto wao kusoma ili siku moja kata zao zitoe viongozi bora wa kuliongoza taifa lakini pia kama mkakati wa kuondoa umasikini kwenye jamii huku akiwaasa viongozi kuacha alama na siyo lawama, wakileta matokeo na siyo matukio.
Wananchi wa kata ya Izumacheli ambacho ni kisiwa nao wakaiomba serikali kuona namna bora ya kuwasaidia upatikanaji wa maji safi na salama ukizingatia uwepo wa wanyama hatari “Mamba” kwenye mwambao wa ziwa wanalolitumia kupata maji, kuwawezesha vyombo vya usafiri majini ili iwasaidie kupunguza gharama ya vifaa vya ujenzi lakini pia ujenzi wa bweni kuepuka wanafunzi kuvuka maji kila watakapoenda shule.
Kwa upande wa kata ya Nkome na Katoma zilipo shule za Mnyala na Katoma sambamba, wameiomba serikali kuzisaidia umeme pamoja na maji safi na salama, suala lilitolewa ufafanuzi na wataalamu wa maji na umeme kwa kuhakikisha kuwa, umeme utayafikia maeneo hayo kuanzia mwezi Julai, 2021 na maji kupatikana kupitia mradi mkubwa wa maji utakaotekelezwa hivi karibuni.
Katika ziara hiyo iliyohudhuliwa na viongozi wa tarafa na kata, wa chama tawala CCM na serikali, mhandisi Gabriel aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Geita Fadhili Juma, mkurugenzi wa halmashauri, wataalam wa sekta ya elimu, afya, maji, umeme na mipango ngazi ya mkoa na wilaya ambao waliweza kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyojitokeza kwenye ziara hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa