Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba, Januari 21, 2025 amefanya ziara katika Kisiwa cha Izumacheli kilichopo ziwa Viktoria Mkoani Geita.
Mhe Komba katika Ziara hiyo, amekagua mradi wa nyumba ya mtumishi zahanati ya Izumacheli pamoja na Mabweni mawili ya shule ya Sekondari Izumacheli ambapo amefanya uzinduzi wa Mabweni hayo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Mabweni ya Wasichana na Wavulana katika shule ya Sekondari Izumacheli, Kaimu Afisa Mtendaji Kata ya Izumacheli Ndg Boniphace Jeremia amesema mradi huo unafadhiliwa na mfuko wa maendeleo wa jamii(TASAF) ambapo jumla ya Kaya 167 zinanufaika toka mwaka 2020 na kiasi cha Shilingi 194,187,000 zimekwisha pokelewa ikiwa ni ruzuku za walengwa wa mpango kuanzia Julai , 2020 hadi Desemba , 2024.
“Ujenzi wa Mabweni mawili yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 48 kila moja ulianza mwaka 2022/23 kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Izumacheli kwa gharama ya Shilingi 203,291,294.79 ambapo asilimia 10 ya gharama za mradi imechangiwa na wananchi” amesema Kaimu Mtendaji huyo katika taarifa ya mradi huo mbele ya Mhe Komba.
Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Izumacheli wakati wa uzinduzi wa Mabweni ya shule ya Sekondari Izumacheli, Mhe Komba amewataka wazazi walezi kuendelea kushikamana na walimu ambao wanafundisha katika Kisiwa hicho “Niwaombe wana Izumacheli muendelee kuwapenda walimu na kuwapa ushirikiano kwani wanafanya kazi kubwa ya kuwainua kitaaluma watoto wetu” Amesema Mhe Komba.
Vilevile amewataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kujiamini ili kufikia ndoto zao kwa kuepuka vitisho mbalimbali wanavyokutana navyo katika safari ya masomo.
Pamoja na hayo Mhe Komba amewataka wananchi kisiwani humo kudumisha amani na utulivu. “Lazima Mlinde amani na utulivu kwa wivu mkubwa na kama kuna mtu mnaona mienendo yake sio mizuri mtoe taarifa ili vyombo vya ulinzi na usalama viweze kuchukua hatua” Amesisitiza Mhe Komba
Aidha Mhe Komba ametoa rai kwa wananchi wa Kisiwa hicho kujiepusha na mambo ambayo yanaweza sababisha migogoro na kisiwa cha Hifadhi ya Rubondo ili kuendelea kulinda ustawi wa wananchi.
Hali kadhalika Mhe Komba ameitaka Halmashauri kuhakikisha Kata hiyo inapata Mtendaji wa Kijiji kufuatia mtendaji aliyekuwa akitumika katika kijiji hicho kuwa tatizo na kupelekea kuwa na malalamiko kwa wananchi na migogoro ya madai na malumbano “Niendelee kuwataka watumishi wa umma na wananchi kuwa na umoja na mshikamano ili kusukuma gurudumu la maendeleo.” Ameongeza Mhe Komba.
Pamoja na hayo Mhe Komba amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kufunga umeme Jua katika Kisiwa hicho ili wananchi wanufaike na kuchochea shughuli za maendeleo.
“Dkt Samia Suluhu Hakuna alichokisahau, tumebaki na vijiji 3 kati ya vijiji 158 vya wilaya ya Geita ambavyo havina umeme, Serikali kupitia Wizara ya Nishati inayo ongozwa na Mhe Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dotto Mashaka Biteko (MB) inafanya kazi kubwa kumpa kazi mtu wa Rea kutafuta mzabuni wa kufunga umeme wa jua utakaosambazwa katika vijiji vitatu ili kukamilisha vijiji vyote vya wilaya ya Geita kuwa na umeme.
Katika Ziara hiyo Mhe Mkuu wa Wilaya aliambatana na Katibu Tawala wilaya Bi Lucy Beda, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Geita pamoja na Wataalam kutoka halimashauri ya Wilaya ya Geita wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Bi Sarah Yohana.
Kisiwa cha Izumacheli ni moja ya Visiwa vitatu ndani ya Izumacheli vyenye makazi ya watu na Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kupekeleka huduma za kijamii zikiwepo shule na zahanati. Visiwa vingine vikiwa ni Butwa, Lulegeya na Kisiwa cha Hifadhi ya Rubondo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa