Na Michael Kashinde
Katika kilele cha maadhimisho miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amewataka wananchi kuendelea kuuenzi muungano uliojengwa kwa misingi ya undugu na kutobaguana ambao umekuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.
RC Shigela ameyasema hayo 28 April, 2023 akiwa katika Kijiji cha Nyakagwe kata ya Butobela Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo alizindua mradi wa bweni la wanafunzi 80 wa kike katika shule ya sekondari ya Nyakagwe, mradi uliogharimu jumla kiasi cha Tshs. 157,084,142.85/=.
Katika mradi huo wa bweni la wasichana RC Shigela ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia CSR na vyanzo vingine vya mapato kuhakikisha wanapeleka magodoro, pamoja na huduma ya umeme na maji katika shule hiyo ili wananchi wasichangishwe, huku akipongeza kazi ya ujenzi huo kusimamiwa vizuri na kwa ubora unaokubalika.
Aidha Mhe. Shigela aliendelea kwa kusema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo watanzania ambapo kwa kipindi cha miaka miwili maendeleo makubwa yameonekana katika sekta zote ambapo kwa mwaka huu pekee tayari kuna bilioni 12 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe akiwahutubia wananchi hao wa kijiji cha Nyakagwe ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi mbalimbali ya Serikali kuwa waadilifu na kutimiza wajibu wao ili kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia ambaye anahangaika kuzitafuta fedha hizo kwa lengo la kuwaletea maendeleo watanzania.
Wakati huo huo ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii kuwalinda watoto wa kike ili kuwaepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri maisha na elimu yao huku akisistiza kuwa Serikali haitawafumbia macho wale wenye tabia ya kuwalaghai kimapenzi wanafunzi wa kike.
Naye mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita Ndg. Barnabas Mapande alisema kuwa fedha ni nyingi zinazotolewa na Rais Samia na zinajenga miradi bora kabisa inayopunguza kero kwa wananchi ikiwemo kwenda shuleni na madawati huku akisistiza kuwa Chama kitaendelea kumuunga mkono kwa kusimamia miradi hiyo kama kama inavyoleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Awali akitoa taarifa ya Mradi wa Bweni la wasichana 80 katika shule ya sekondari Nyakagwe Afisa Mtendaji wa kata ya Butobela Ndg. Reuben Malume Makala alisema kuwa mradi huo uliojengwa kwa jumla ya Tshs. 157,084,142.85/=, 10% ya fedha za mradi huo ambayo ni Tshs.17,550,000.00/= imechangiwa na wananchi huku kiasi cha Tshs. 139,534,142.85 ikitolewa na mfuko wa maendeleo (TASAF).
Mradi huu unatajwa kuondoa au kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike shuleni kutokana na changamoto za mimba za utotoni na kutembea umbali mrefu kuhudhuria masomo ambapo kukamilika kwake kunatazamiwa kuongeza hali ya ufaulu kwa watoto wa kike shuleni.
Mradi huo licha ya kuwajengea uwezo kamati ya usimamizi ya jamii hususani katika masuala ya usimamizi na manunuzi ya mradi kwa ujumla lakini pia mradi huo umetoa ajira mbalimbali za ufundi ujenzi, huduma za vifaa na chakula kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali hali iliyoongeza mzunguko wa fedha kwenye jamii.
Kupitia mradi huo Serikali ya kijiji cha Nyakagwe imetoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya Sita pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuboresha miundombinu ya kutolea elimu katika shule ya sekondari Nyakagwe hali itakayoongeza ufaulu wa wanafunzi na kuondoa utoro shuleni hususan kwa watoto wa kike.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa