Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa imeahidi kuunga mkono kwa kiasi cha shilingi milioni moja ujenzi wa Mradi wa kituo cha Afya Busanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita unaotekelezwa kutokana na nguvu za wananchi, wadau wa maendeleo na mfuko wa jimbo.
Katibu Mkuu wa jumuiya ya wazazi CCM Taifa Ndg.Gilbert Kalima akiwa katika ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa katika jimbo la Busanda Novemba 17, 2021 ameahidi kiasi cha shilingi Milioni moja kuunga mkono ujenzi wa Mradi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndg.Daniel Chongolo.
Akiwa katika kata ya Busanda mara baada ya kupewa taarifa ya Mradi huo Kalima amewataka wanaCCM kuendelea kuwahamasisha wananchi kujitolea kwa nguvu na mali kufanikisha ujenzi wa Mradi huo kwa faida ya wakazi wa kata ya Busanda ambayo hadi sasa haina kituo cha Afya zaidi ya zahanati mbili zinazofanya kazi.
Aidha Ndg.Kalima ametoa rai ya kuwa na mikutano ya mara kwa mara ya kujadiliana na kufikia maamuzi ya pamoja sambamba na kupeana taarifa za wazi za fedha ili kuepusha migogoro inayoweza kukwamisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Busanda Mhandisi Tumaini Magesa amesema kuwa tayari imekwishatolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuchimba barabara inayounganisha Busanda, Kirungure, Buyagu, na Rwamgasa huku akiahidi kuwafuatilia kwa karibu wakandarasi ili barabara hizo zisiwe chini ya kiwango.
Naye diwani wa kata ya Busanda Mh.Selemani Gamala amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza katika kata hiyo Miradi ambayo haikuwahi kutekelezwa kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupewa fedha kiasi cha shilingi milioni 210 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 10 kwenye kata hiyo, sambamba na milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha zahanati, huku akieleza changamoto ya umbali wa Halmashauri katika kuwapatia huduma wananchi wa kata hiyo.
Awali akitoa taarifa ya Mradi huo Mtendaji wa kata ya Busanda Bi.Victoria Mapunda amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha Afya ulianza rasmi mwaka 2017 ambapo kwa sasa uko katika hatua ya ufungaji wa lenta ya kwanza ukiwa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 23 laki 2 na elfi 1 zilizotumika kununua vifaa mbalimbali vya ujenzi pamoja na gharama za ufundi.
Kata ya Busanda inayoundwa na vijiji vinne vyenye jumla ya vitongoji 15 na wakazi wapatao elfu 23 mia 8 na 47, inakabiliwa pia na changamoto ya maji safi na salama na nishati ya umeme katika vijiji vyote hivyo vinne, ingawa kuna Mradi mkubwa wa umeme wa gridi ya Taifa ambao unaanzia Mpomvu Geita kuelekea Nyakanazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa