Watumishi wa Umma na wadau wa Maendeleo Mkoani Geita , leo Mei 13, 2025 wamepatiwa mafunzo ya kuzuia Rushwa.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg.Mohamed Gombati amebainisha Kuwa rushwa ni adui wa haki,usawa na maendeleo katika jamii.
Ndg.Mohamed Gombati ameyabainisha hayo alipokuwa akifungua Warsha ya wadau kuhusu uzuiaji wa rushwa iliyoandaliwa na TAKUKURU wakishirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGML) katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Aloysius, Manispaa ya Geita.
RAS Gombati amesema lengo la Warsha hiyo ni kujadili,kuandaa mkakati wa namna bora ya kukabiliana na rushwa au viashiria vya rushwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo zinafanywa na kutekelezwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML)
Ndg.Mohamed Gombati ameongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la jamii kwa ujumla na sio TAKUKURU pekee.
" Eneo lolote lenye viashiria ama mazingira ya Rushwa Linarudisha nyuma utoaji wa huduma zetu, kupunguza kasi ya kukua kwa uchumi katika eneo hilo na kuathiri mazingira ya uwekezaji na biashara" Amesema Katibu Tawala Mkoa wa Geita.
Kwa Upande Wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, Denis Lekayo amesema TAKUKURU imekabidhiwa sheria ya kudhibiti na Kupambana na rushwa kwa kuweka mifumo rafiki ya utoaji taarifa na kusimamia haki za binadamu Mkoani Geita
Aidha ametoa wito kwa wakuu wa taasisi kutoa ushirikiano wa kuchangia uzoefu,kubadilishana taarifa na kuweka rasilimali za kazi pamoja ili Kupambana na adui rushwa Mkoani Geita kwa lengo la kuinua sekta ya madini kwa kushirikiana na mgodi wa dhahabu wa Geita.
" Watumishi wa Umma ni wawakilishi wa Serikali na wanatakiwa kuwa mfano wa uadilifu katika utekelezaji wa Majukumu yao" Amesema Lekayo.
Warsha hiyo inayotarajiwa kufanyika kwa siku mbili Mkoani Geita inaongozwa na kauli mbiu isemayo"kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu tutimize wajibu wetu"
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa