Na. Michael Kashinde
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani Disemba 1, 2022 amewataka wananchi kuitumia siku hiyo kutafakari namna ya kupambana na Ugonjwa wa UKIMWI kwa kuwa ni moja ya ugonjwa hatari duniani ambao hauna chanjo wala dawa ya kuutibu.
Akiwa katika viwanja vya Kakubilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita yalipofanyikia maadhimisho hayo Kimkoa, RC Shigela amesisitiza kuwa ni lazima kila mmoja aweze kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI ambapo pia ametumia nafasi hiyo kueleza madhumuni ya siku ya UKIMWI duniani kuwa ni kukumbushana UKIMWI bado upo, na ni fursa pia ya kuwakutanisha wadau na Serikali kueleza mipango iliyopo ya kuhakikisha ugonjwa wa UKIMWI unatokomezwa.
Aidha RC Shigela ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupata Elimu ya ugonjwa wa UKIMWI na kipima ili kujua Afya zao, sambamba na kuanza kutumia dawa mara tu mtu anapogundulika kuwa na maambukizi huku akiongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha huduma hizo kwa kutoa vipimo na dawa bure kwa kuwa ni Serikali inayojali Afya za watanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akizungumza katika maadhimisho hayo ameendelea kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari zote za kujinga na virusi vya UKIMWI kwa kuwa taarifa zinaonyesha UKIMWI bado upo, huku akiwataka wananchi hao pia kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Chanjo ya Polio linaloendelea kuanzia leo hadi Disemba 4 likiwalenga Zaidi watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.
Awali Akizungumzia hali ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Mkoa wa Geita Dkt. Yohane Kihaga Kaimu Mratibu wa kupambana na Virusi vya UKIMWI mkoa wa Geita amesema kuwa matokeo ya tafiti ya mwaka 2016 na 2017 yanaonyesha kuwa wastani wa maabukizi katika Mkoa wa Geita ni 5% ambapo hali ya sasa ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini inaonyesha kuwa 40% ya maambukizi yote ni vijana ambapo 80% ya vijana hao ni wa kike.
Kwa upande wa hali ya jumla ya kijinsia na kiumri inaonyesha kuwa kuna maambukizi makubwa kwa wanawake kuliko wanaume ambapo pia afua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kudhibiti maambukizi ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu kwa jamii ya kujinga na virusi vya UKIMWI, kuepuka mila potofu dhidi ya ugonjwa huo na kuhamasisha jamii kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ingawa wanaume wanatajwa kuwa na mwitikio mdogo zaidi wa kupima ili kujua Afya zao ikilinganisha na wanawake.
Naye Bi. Patricia Nsinde Mratibu wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita amesema kuwa katika Afua ya Huduma na matunzo kwa mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetumia kiasi cha milioni 22 na laki 2 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kulipia BIMA ya Afya iliyoboreshwa kwa Kaya 740.
Aidha katika kutekeleza Afua hiyo ya huduma na matunzo Halmashauri ya Wilaya ya Geita Disemba Mosi, 2022 imetoa msaada wenye thamani ya shilingi Milioni 4 Laki 4 na elfu 20 kwa ajili ya kuhudumia watoto 66 waliobainishwa kuwa wanalelewa katika mazingira magumu ambapo kila mmoja amepatiwa mashuka manne, kilo sita za chakula, miche 6 ya sabuni, na ndoo kwa ajili ya kutumia kutunzia maji ya kunywa kwenye kaya ambapo Mgeni Rasmi RC Shigela amekabidhi misaada hiyo.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani mwaka huu yameambatana na kauli mbiu isemayo “Imarisha Usawa” ambapo huduma mbalimbali na elimu imekuwa ikitolewa katika mabanda maalumu yaliyoanza kuhudumia wananchi tangu Novemba 28, 2022 ambapo hii leo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela alipata nafasi ya kutembelea mabanda hayo na kusikia kutoka kwa wataalamu huduma zinazotolewa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa