RC Senyamule ametoa wito huo wakati akihutubia wafanyakazi na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi Duniani Meimosi, 2022 yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya Kalangalala mjini Geita Mhe. Senyamule akiwa mgeni rasmi.
Akijibu risala ya Wafanyakazi iliyogusia changamoto mbalimbali zinazowakabili Mhe. Senyamule amesema kuwa changamoto zinaihusu Serikali zimesikilizwa na zitafanyiwa kazi kwa kuwa Serikali ni sikivu na inaheshimu Misingi ya Utawala bora.
Aidha ametoa wito kwa waajiri wote katika Mkoa wa Geita kuzingatia Sheria, miongozo, na taratibu za utumishi wa Umma pale wanaposhughulikia masuala ya kinidhamu kwa watumishi ili kuepuka udhalilishaji kwa watumishi sanjari na kuwakumbusha watumishi kuzingatia maadili ya kazi zao.
RC Senyamule ametumia pia fursa hiyo kukemea tabia ya baadhi ya watu kuwatumikisha watoto kwa kuwafanyisha kazi za nguvu zenye ujira mdogo na usiokidhi haja zao huku akisema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kutoa wito kwa makundi mbalimbali vikiwemo vyombo vya dola kupinga suala hilo kwa kuwa haki ya mtoto ni kupewa Elimu pekee.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amewataka watumishi kuunga mkono juhudi za Mtumishi namba moja nchini Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kwa bidii na kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi.
Aidha Mhe. Shimo amesisitiza kuwa mafao na maslahi ya watumishi yanajengwa na wajibu wao ambao wanautimiza kila siku, huku akiwakumbusha kuzingatia uchapakazi, uadilifu, na weledi ili malengo yao ya kupata maslahi zaidi yawezekane kwa urahisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg. John Wanga amesema kuwa Kauli mbiu ya ''Mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ndiyo kilio chetu kazi iendelee'' kwa Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa haiwafanyi wakapoteza lengo lao kuu la kuwatumikia watanzania katika sehemu zao za kazi huku akiwapongeza kwa kuupiga mwingi katika kutekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi Wanga ameendelea kusema kuwa Sikukuu ya Meimosi inawakumbusha watumishi duniani kote kutafakari majukumu yao katika nafasi zao mbalimbali, huku akitoa wito wa kumuunga mkono Mhe. Rais katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/2025 iliyolenga kuwaletea huduma bora Wananchi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa TALGWU Ndg. David Mhagama amesema kuwa watumishi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama maslahi duni, kuchelewa kwa mafao ya watumishi, na kutokukaa kwa mabaraza ya wafanyakazi huku Serikali ikishauriwa kudhibiti mfumuko wa bei ili kupunguza gharama za maisha kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.
Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani katika Mkoa wa Geita yamepambwa na burudani na michezo kutoka vikundi mbalimbali ndani ya mkoa wa Geita huku Mgeni rasmi akikabidhi zawadi kwa wafanyakazi bora wa Umma, taasisi na mashirika mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa