Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amepongeza hatua ya mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Samia Suluhu Hassan inayojengwa katika eneo la Mtakuja lililopo katika kata ya Katoro kwa gharama ya shilingi milioni mia nne na sabini.
Akiwa katika ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita April 25, 2022 Mhe. Senyamule ametembelea mradi huo uliopewa jina la Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kutambua mchango wake katika miradi ya huduma kwa wananchi, ambapo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kusimamia vizuri mradi huo unaoendelea kwa kasi huku akishauri kuongeza nguvu zaidi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Akitoa taarifa ya Mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Katoro George Hezron amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Januari 28, 2022 ukiwa na jengo la utawala maktaba, jengo la Tehama, matanki mawili ya maji, majengo matatu ya maabara za kemia, fizikia, na bailojia.
Aidha majengo mengine ni matundu 20 ya vyoo, ujenzi, wa sehemu ya kunawia mikono na vyumba 8 vya madarasa, ambapo mradi huo ukikamilika unatarajiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya sekondari Katoro.
Awali Mhe.Senyamule alianza ziara yake kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Katoro inayojengwa kwa gharama ya Tshs. bilioni 2.2 kutoka Serikali kuu iliyoelekezwa katika vifaa na majengo ya kitengo cha matibabu ya dharura, wodi za magonjwa ya wanaume na wanawake.
Aidha majengo mengine ni pamoja na wodi ya watoto, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kuchomea taka, uzio, na nyumba za watumishi 3 kwa 1.
Mhe. Senyamle baada ya kuzungumza na mafundi ili kufahamu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, akatoa wito kwa Halmashauri zote kutoa fedha kwa wakati ili mafundi wasikwame kuendelea na kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali wanayokuwa wamepewa kwa kusubiri fedha.
wakati huo huo ametoa wito kwa mafundi hao ambao ni sehemu ya jamii kutumia vyema fursa waliyoipata kwa kujenga miradi bora na kuimaliza kwa wakati uliopangwa, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama wa vifaa na miundombinu hiyo kwa ujumla ili iwanufaishe wananchi kama Serikali inavyokusudia.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa Hospitali ya Katoro Eng. Khamis Abeid Ngonde ameahidi kuongeza nguvu kazi, na kufikia April 28, watakuwa wameshafunga taa kwa ajili ya kufanya kazi usiku na mchana ili Mradi huo ukamilike kabla ya May 30, 2022 kama alivyoagiza Mhe. Mkuu wa mkoa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa