Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa hatua iliyofikia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia fedha za Uviko 19.
Akiwa Mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania yaliyofanyika katika Wilaya ya Geita Decemba 7, 2021 katika shule ya Sekondari Nyamigota Senyamule amekagua na kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa ujenzi wa vyumba sita (6) vya madarasa katika shule ya sekondari Nyamigota.
Aidha amepongeza hatua ya Mradi huo na mingine inayoendelea kujengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita huku akitoa wito kwa wazazi kuwafuatilia watoto wao ili waende shule na wasome kwa bidii kwa kuwa matarajio ya Mheshimiwa Rais Samia ni kuona ufaulu unaongezeka kutokana na uwepo wa madarasa ya kutosha.
Aliendelea kusema kuwa tunaposherehekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania ni vyema kila mwanajamii akatimiza majukumu na wajibu wake ili kufikia matarajio ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuona uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Mradi wa huo Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamigota Mwalimu Sosthenes Ilagila alisema kuwa shule hiyo ilipata kiasi cha shilingi milioni mia moja ishirini (120,000,000) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa ambapo ujenzi ulianza rasmi novemba 11, 2021 ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia 80%.
Aidha aliendelea kusema kuwa Mradi huo ukikamilika utaongeza ufaulu zaidi kwa kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia na pia kuondoa uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa hatari wa UVIKO 19 kwa kuwa wanafunzi na walimu wataweza kukaa kwa umbali unaoelekezwa na wataalamu wa Afya.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mheshimiwa Charles Kazungu ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa kuiheshimisha Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuipatia bilioni 7 na milioni 940 kwa ajili ya Miradi hiyo ya Elimu na Afya.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa