Geita-Tanzania
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Ndg Mohamed Gombati, Agosti 12, 2025 ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru Septemba 01,2025 katika Halmshauri ya wilaya ya Geita.
Katika ziara hiyo Ndg Gombati ametembelea miradi ya afya,elimu pamoja na barabara ikiwemo sehemu ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya shule ya sekondari ya Lwezera iliyopo kata ya Lwezera.
Katibu Tawala huyo ametembelea na kukagua miradi hiyo itakayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa ufanisi mkubwa.
Pamoja na hayo Ndg Gombati ameagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini(TARURA) kuhakikisha miundombinu ya barabara inarekebishwa ili ziendelee kudumu na zitumike kwa ufanisi.
Pia katika Ziara hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Geita amepongeza uongozi wa hospitali ya Nzera kwa kukamilisha ujenzi wa majengo mapya ya hospitali kwa wakati uliopangwa. Majengo haya ni mojawapo ya miradi mikubwa itakayozinduliwa rasmi wakati wa Mwenge wa Uhuru.
Vilevile Ndg Gombati ametoa agizo kwa wahusika wote wanaosimamia miradi ya maendeleo kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa wakati uliopangwa ili kuepuka adha na changamoto zitakazoweza kuathiri uzinduzi wa miradi hiyo huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi makini ili miradi hiyo itekelezwe kwa mafanikio kama ilivyopangwa.
Aidha, Ndg Gombati amewasisitiza viongozi wote kuwahimiza wananchi wote kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita kushiriki kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaokimbizwa Septemba 01, 2025.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa katika viwanja vya shule ya Sekondari-Lwezera kata ya Lwezera ukitokea Mkoa wa Mwanza na baadaye kukimbizwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kufatiwa na Mkesha katika viwanja vya shule ya Msingi Ludete na baadaye kukabidhiwa Manispaa ya Geita Shule ya Msingi Shanta Mine-Mpomvu.
Mwenge wa Uhuru umebebwa na Kauli mbiu: Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa