Na: Hendrick Msangi
MKUTANO wa kawaida wa baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita, May 9, 2024 umeendelea kwa uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa Shughuli za Serikali ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha Januari hadi Machi.
Katika Kikao hicho kamati za kudumu za Halmashauri zimewasilisha taarifa zake kwa kipindi cha Januari hadi Machi ikiwa ni pamoja na kujibu maswali kutoka kwa wajumbe wa baraza hilo kwa mujibu wa kanuni ya 22 ya kanuni za kudumu za Halmashauri.
Kamati zilizo wasilisha taarifa za utekelezaji wa Shughuli za Serikali ni pamoja na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na mazingira, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, na Kamati ya Maadili.
Madiwani hao wameonyesha kukereka na swala la CSR kwa namna utekelezaji wake unavyoendelea .Wakizungumzia miradi inayotekelezwa na Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) madiwani hao wamesema swala la CSR limekuwa ugonjwa unaowatafuna katika kata zao na kuazimia kuwa na baraza maalumu kwa ajili ya kujadili miradi ya CSR ambayo imekuwa viporo kwa muda mrefu.
Aidha madiwani hao wametaka miradi inayotekelezwa na nguvu za wananchi kupewa kipaumbele ili kukamilika kwa wakati na kwa ubora huku wakitoa agizo uwepo wa wahusika wa miradi kutoka mgodi wa dhahabu wa GGML kushiriki vikao vyote ikiwepo baraza ili kutoa majibu kwa waheshimiwa madiwani juu ya miradi wanayoitekeleza.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Geita,Gabriel Nyasilu amelipongeza baraza la madiwani kwa namna walivyo endesha kikao cha baraza hilo na ushirikiano walio nao katika kufanya kazi kuleta matokeo mazuri katika kufikia malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha Cde Gabriel amepongeza maamuzi yaliyofanywa na baraza hilo kwa kutokuuza mitambo ambayo haijafanya kazi muda mrefu kutokana na ubovu. “Tumeridhishwa na maamuzi yenu ya kutokutaka kuuza mitambo, fanyeni jitihada ili itengenezwe iweze kusaidia changamoto za barabara katika kata.” Amesema Cde Gabriel.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dkt Alphonce Bagambabyaki amesema Halmashauri itatekeleza yale yote yaliyoazimiwa na baraza hilo ikiwa ni pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka vizuizi katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti utorashaji wa mazao hasa nyakati za usiku.
"Tutakuwa na Baraza Maalumu kwa ajili ya kujadili Miradi ya CSR ambayo imekuwa viporo Kwa muda mrefu, kwani suala la CSR limekuwa ugonjwa unaotutafuna" Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akifunga Kikao cha Baraza hilo la robo ya tatu, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Charles Kazungu ametoa rai kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuendelea kufanya kazi kwa kujituma huku wakiyatimiza yale yote ambayo baraza limeazimia katika kutimiza wajibu wao.
"Watumishi Ongezeni bidii katika ukusanyaji wa mapato ili Halmashauri iweze kufanya shughulizi zake" Mhe Charles Kazungu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Aidha Mhe Kazungu, amewasisitiza watumishi kuendelea kuweka bidii katika ukusanyaji wa mapato kwa kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato na kutoa agizo kwa watendaji wote ambao hawafanyi vizuri katika ukusanyaji wa mapato kunyang’anywa mashine za kukusanyia ushuru(Pos) na kuwapa watu wengeine ambao watakusanya kwa bidii kwani wapo watendaji ambao wanachelewesha kwa makusudi kubenki fedha za mapato.
“ Mimi ni Muumini wa mapato hivyo mapato yakusanywe ili Halmashauri iweze kujiendesha na tukasimamie shughuli za maendeleo katika kata zetu ili fedha zinatolewa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilete matokeo na pia mkumbuke kusoma mapato na matumizi katika maeneo yenu ” alisema Mhe Kazungu
Mhe Kazungu amewashukuru waheshimiwa madiwani kwa michango yao katika baraza hilo na kuendesha baraza kwa muda mfupi huku akiwapongeza wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri kwa namna walivyotoa ushirikiano katika kufanikisha baraza hilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa