Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Magaro, ametembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika kata za Nkome, Lwenzera, na Nzera, ndani ya halmashauri hiyo. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukagua maendeleo ya zoezi hilo muhimu.
Akiwa katika kata ya Nzera, Magaro alijisajili katika daftari la wapiga kura kama sehemu ya kutekeleza haki yake ya kikatiba. Katika ziara hiyo, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhamasishana na kujitokeza kwa wingi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27, 2024.
Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri Ndg. Karia Magaro (kushoto) akionesha alama ya kidole baada ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika Kata ya Nzera.
Magaro aliwakumbusha wananchi kutofautisha kati ya kujiandikisha kuwa mpiga kura kwa ajili ya serikali za mitaa na kuhuisha taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura, ambalo litatumika katika uchaguzi wa serikali kuu wa mwaka 2025.
Wananchi wasichanganye kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na zoezi lililotangulia la kuboresha taarifa za mpiga kura katika daftari la kudumu la mpiga kura, zoezi hili la sasa ni maalumu kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo kila mwananchi bila kujali alijiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura au hakujiandikisha anahaki na wajibu wa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika kitongoji chake ili aweze kuchagua viongozi wa ngazi ya kijiji ifikapo Novemba 27,2024, Alisema Magaro.
Msimamizi wa uchaguzi ngazi ya Halmashauri Ndg. Karia Magaro (katikati) akiwaelezea jambo waandikishaji pamoja na mawakala wa vyama vya siasa alipotembelea kituo cha uandikishaji wapiga kura katika kata ya Nzera
Kwa siku ya kwanza ya zoezi hilo, zaidi ya watu 500 walijiandikisha katika kata za Nkome, Nzera, na Lwenzera. Idadi ya waliojiandikisha inatarajiwa kufika zaidi ya elfu tano kabla ya kukamilika kwa zoezi hilo.
Msimamizi wa Uchaguzi Ndg Karia Magaro (wa kwanza kulia) akichukua taarifa za wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika orodha ya mpiga kura katika kata ya Katoro, wengine pichani ni mwandikishaji wapiga kura pamoja na mawakala wa vyama vya siasa
Uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba 27, 2024, unafanyika chini ya kauli mbiu inayosema, "Serikali za Mitaa ni Sauti ya Watu; Jitokeze Kushiriki Uchaguzi."
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa