Na Hendrick Msangi.
MKUU wa Mkoa wa Geita, Mhe Martine Shigela, Desemba mosi amekabidhi zawadi kwa watoto wanaoishi kaya masikini na zile ambazo zimeathiriwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Zawadi hizo zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni pamoja na Sukari kilo 150, Mashuka pisi 150, sabuni za miche 300, daftari boksi 10 na kalamu boksi 4 ambazo zitagawanywa kwa uwiano sawa kwa kila tarafa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikiwa ni sehemu ya kuonyesha kuwajali na kuwathamini watoto wanaoshi katika kaya hizo.
Baadhi ya zawadi zilizokabidhiwaa na Mhe Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela kwa ajili ya kupelekwa kwa Kaya Masikini ambazo zimekumbwa na janga la Ukimwi Katika Halmashauri ya wilaya ya Geita.
Katika Maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu “Jamii iongoze kutokomeza Ukimwi” ambayo Mkuu huyo wa mkoa alikuwa mgeni rasmi, alisema Mkoa wa Geita ni Mkoa wenye muingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali kutokana na fursa zinazopatikana mkoani humo ikiwemo ya upatikanaji wa madini ya dhahabu, ziwa viktoria, kuingiliana na nchi jirani hivyo aliwaasa wananchi kutumia maadhimisho hayo kukumbushana walipo toka, walipo na wanapoelekea katika kujikinga na janga la Ukimwi.
Aidha alizishukuru taasisi na wadau mbalimbali yakiwepo mashirika kama MDH, Icap, hospitali Pamoja na viongozi wa dini kwa kuendelea kukumbusha jamii dhidi ya janga la ukimwi na kuitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kupima na kujitambua ili kuweza kuweka mikakati ya namna ambavyo jamii itakabiliana na ugonjwa huo wa upungufu wa kinga mwilini.
“Tuyatumie maadhimisho ya siku ya ukimwi kupeana elimu kuwa ugonjwa upo, bado una ambukiza na bado unaua na hivyo ni vema wananchi tukatumia nafasi hii kujifunza na kuweka tafakuri itakayotusaidia dhidi ya kujikinga”, alisema Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo aliwaasa wananchi kutokuupa nafasi Unyanyapaa kwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini kwani haukubaliki na kusema mapambano dhidi ya ukimwi ni kwa jamii yote kwa kuhakikisha wale ambao wameambukizwa wanapewa kila aina ya nasaha, kuwasaidia kifikra, kimawazo ili waeze kuishi miaka mingi zaidi na wasikate tamaa.
Kwa takwimu za mwaka 2022 kiwango cha mambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa mkoa wa Geita kilikuwa ni asilimia 5.1 na kwa mwaka 2023 takwimu zinaonyesha kiwango cha maambukizi ni asilimia 4.7 hii ikiwa na maana maambukizi bado yapo hivyo ni vema kujipanga kwa kuweka mikakati ya kuweza kuondokana na janga hilo la upungufu wa kinga mwilini.
Serikali imejiwekea malengo ifikapo mwaka 2030, asilimia 95 ya wenye maambukizi wafahamike kwa nchi nzima na kwa mkoa wa Geita asilimia 89 ya wananchi wawe wamezifahamu afya zao huku akiwashukuru wote ambao wamejitokeza kwa ajili ya kupima afya zao, kwani serikali imejiwekea malengo ya kupunga maambukizia mapya. Alisema Mhe Shigela.
Pamoja na hayo Mhe Mkuu wa Mkoa aliwasihii watoa huduma za afya kuendelea kuwapenda wagonjwa na kuwajali kwani ndio kimbilio lao, Viongozi wa dini kuendelea kuwakumbusha waumini kila mara wanapokwenda kwenye misikiti na makanisani mapambano dhidi ya ukimwi ili kuepuka maambukizi mapya, wanasiasa kupitia mikutano yao ya hadhara na ya ndani kuendelea kuwakumbusha wananchi ikiwa ni pamoja na kuifanya kuwa ajenda ya kudumu , walimu mashuleni wanapofundisha waendelee kuwakumbusha wanafunzi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa shukrani zake kwa Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujiwekea malengo ya kuhakikisha wale wote waliopata maambukizi wanapata madawa, kuendelea kuboresha sekta ya afya hususani kwenye madawa, vifaa tiba, kuongeza waganga na wauguzi ikiwa ni sehemu ya kuondokana na changamoto za tiba na afya katika Taifa letu.
Mwisho aliwasihi wananchi wa Mkoa huo kuendeleaa kumuombea Rais kuwa na afya njema na maisha marefu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa ajili ya maisha ya Watanzania.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa