Watanzania waliopata Dhamana ya kuajiriwa katika kampuni za kigeni hapa nchini, wameshauriwa kutuwakilisha vyema kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa, ili kujenga Imani kwa waajiri wao, suala litakaloshawishi kampuni hizo kuendelea kuwaajiri watanzania wengine zaidi.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh.Rosemary Senyamule akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya Backreef,inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika kata ya Lwamgasa, akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Amewataka watanzania wanaofanya kazi katika kampuni hiyo kutojihusisha na uzembe ,uvivu na wizi mambo yanayoweza kutuchafua,huku akiwataka kuongeza uwajibikaji, hali itakayoongeza uzalishaji na mapato, kwa kuwa serikali inapata mgawo wa zaidi ya 40% katika mgodi huo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameahidi kuwapa ushirikiano kampuni hiyo na wawekezaji wengine watakaojitokeza, huku akiwashukuru kwa kuwasilisha mchango wao kwa ajili ya maonyesho ya madini, ambayo yanatarajiwa kuanza septemba 16.
Aidha Mh.Senyamule amehitimisha kwa kuwakumbusha kuchukua tahadhari zote zinazoshauriwa na wataalamu wa afya, katika kujikinga dhidi ya mambukizi ya virusi vya korona,huku akisisitiza kuwa vituo vya kutolea chanjo bado viko wazi, na chanjo bado inatolewa kwa yeyote atakayehitaji huduma hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa