Wasimamizi wa vituo na Makarani waongozaji kutoka Jimbo la Geita na Busanda wamepewa mafunzo katika kuwajengea uwezo kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Bomani Geita kwa wasimamizi wa Jimbo la Geita huku Jimbo la Busanda wakipewa mafunzo katika ukumbi wa shule ya Sekondari Butundwe ambapo wasimamizi na makarani hao wamepewa mafunzo namna ya kusimamia zoezi zima la uchaguzi ili wawapo katika vituo waweze kusimamia na kuzingatia kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro akizungumza na Wasimamizi wasaidizi na Makarani katika Ukumbi wa Mikutano Bomani-Geita ambapo amewataka kuwa waadilifu katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27.
Akizungumza katika mafunzo hayo Msimamizi Msaidizi Ndg Juma Chota amewasihi Makarani na wasimamizi wasaidizi hao kuzingatia taratibu na kanuni zote kwa mujibu wa muongozo wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji.
Pamoja na mafunzo hayo, wasimamizi wasaidizi na makarani hao wameelekezwa taratibu zote za upigaji kura, sifa za wapiga kura na vifaa vitakavyotumika katika zoezi zima la upigaji kura.
Akifunga mafunzo hayo Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajabu Magaro amewataka wasimamizi wasaidizi na makarani hao kupitia mafunzo waliyopewa kufuata kanuni na taratibu za muongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili zoezi la Uchaguzi liweze kwenda vizuri.
Wasimamizi wasaidizi na Makarani waandikishaji wakiwa kwenye mafunzo katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Butundwe ambapo wameaswa kusimamia kwa uadilifu zoezi zima la uchaguzi ili wananchi waweze kushiriki vema zoezi hilo na wasiwe sehemu ya changamoto katika uchaguzi huo
“Tusiwe wabinafsi kama jambo hulielewi uliza kwa viongozi wako ili mzingatie kanuni zilizowekwa na kuwa makini kuepuka kushurutishwa na mtu yeyote wakati wa zoezi zima la Uchaguzi” amesema Magaro.
Aidha Magaro amewataka wasimamizi wasaidizi na makarani hao kulinda dhamana walizopewa kwa kuaminiwa katika zoezi zima la Uchaguzi.”Tuzingatie kuwahi mapema kwenye vituo ili kuhakikisha maandalizi yote yapo vizuri ili saa mbili Wananchi waanze kupiga kura hadi saa kumi jioni ili kama Halmashauri zoezi liweze kwenda vizuri” ameongeza Magaro.
Wasimamizi wasaidizi na Makarani waandikishaji wakiwa kwenye mafunzo katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Butundwe ambapo wamekula kiapo cha utii, uadilifu na uaminifu mbele ya Mkurugenzi Mtendaji Ndg Karia Magaro Novemba 23, 2024
Pamoja na mafunzo hayo wasimamizi wasaidizi na makarani hao wamekula kiapo cha utii, uadilifu na uaminifu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Geita Mhe Devotha Kasebele.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina majimbo mawili ya Uchaguzi yenye Kata 37, Vijiji 145 na Vitongoji 593 ambapo jumla ya vyama 7 vya Siasa ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendelo(CHADEMA), ACT WAZALENDO, CCK, TLP na ADC vitashiriki Uchaguzi huo Novemba 27, 2024.
Wasimamizi wasaidizi na Makarani waandikishaji wakiwa kwenye mafunzo katika Ukumbi wa Halmashauri Bomani-Geita ambapo wamekula kiapo cha utii, uadilifu na uaminifu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Geita Mhe Devotha Kasebele. Novemba 22, 2024
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa