Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Geita, Ndg. Karia Magaro, amewataka walimu wilayani humo, kuongeza juhudi ili kukabiliana na kukithiri kwa changamoto ya Utoro wa wanafunzi, ili kuweza kuinua sekta ya Elimu Wilayani Geita.
Akizungumza tarehe 4, Juni wakati wa ziara maalumu ya Mpango Kazi wa Ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo katika Kata za Bugulula, Isulwabutundwe, Kamhanga na Lubanga, ambapo aliongozana na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Magaro amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa suala la Elimu nchini linapewa kipaumbele kwa kuboresha miundombinu haswa upande wa madarasa, pamoja na kujenga nyumba mpya na za kisasa kwa watumishi.
Ndg. Magaro ameongeza kuwa, Walimu wanao wajibu wa kuhakikisha wanachukua juhudi za makusudi ili wanafunzi waweze kuhudhuria masomo pasi na kukosa, badala ya kujiingizi katika shughuli nyingine za kijamii kipindi cha masomo.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sekondari, Mwl. Hosana Nshullo amekiri kuwepo kwa changamoto ya mdondoko (Dropout) miongoni mwa wanafunzi Wilayani humo hivi karibuni, lakini juhudi zinafanyika ikiwemo kushirikiana na Wazazi, kupitia kwa Watendaji wa Kata ili kuongeza ari ya kujifunza kwa wanafunzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa