Na Hendrick Msangi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Kata za Halmashauri hiyo kwa fedha zinazotolewa kutoka Serikali Kuu kupitia SEQUIP.
Shule ya sekondari ya Samia iliyopo kata ya Katoro ni moja ya shule ambayo inajengwa kwa fedha za SEQUIP na kwa sasa shule hiyo imekamilisha mradi wa jengo la mtumishi (2 in 1) kwa gharama ya shilingi milioni mia moja.
Nyumba ya Watumishi iloyojengwa kwa fedha za SEQUIP kiasi cha shilingi milioni mia moja. Nyumba hiyo ipo kwenye hatua za ukamilishwaji.
Nyumba hiyo yenye ubora imefikia hatua za mwisho ambapo walimu wataweza kuingia na kupunguza gharama na umbali wa sehemu wanazoishi.
Shule hiyo yenye jumla ya madarasa nane ambayo yamekamilika ina jumla ya wanafunzi 321 wa kidato cha kwanza na walimu 15, na kwa sasa serikali imeelekeza fedha kwa ajili ya ukamilishwaji wa majengo ya maabara 3, maktaba 1 na jengo moja la Tehama.
Ujenzi wa Majengo ya Maabara na Maktaba shule ya Sekondari Samia unaendelea. Kwa sasa Shule ya Sekondari Samia ina wanafunzi wa kidato cha kwanza 321
Mradi mwingine wa shule ambao upo kwenye hatua za ukamilishwaji ni shule ya sekondari iliyopo kata ya Ludete ambayo ina jumla ya madarasa 8, jengo la utawala 1, Tehama 1 maktaba 1 na maabara tatu za masomo ya sayansi na matundu 8 ya vyoo wenye gharama ya kiasi cha shilingi 584,280,029 ambapo mwezi januari unatarajia kupokea wanafunzi wasiopungua 300 wa kidato cha kwanza.
Majengo ya Madarasa ya Sekondari kata ya Ludete Wilayani Geita yakiwa katika hatua za ukamilishwaji ambapo Mwezi Januari 2024, shule hiyo itapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wasiopungua 300.
Pamoja na hayo wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wake ndugu Karia Rajabu Magaro wamekuwa wakitembelea mara kwa mara miradi hiyo na kutoa maelekezo kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo pamoja na wasimamizi wa shule hizo kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kwa ubora ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuweza kuhudumia jamii kwa kuhakikisha mafundi wa kutosha wanakuwa kwenye miradi, ulipwaji wa fedha kwa wazabuni na wakandarasi kwa wakati ili kusiwepo na sababu za kuchelewesha miradi hiyo kwani tayari fedha zimeshaelekezwa kwenye miradi hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndugu Karia Rajabu Magaro akikagua Ujenzi wa shule ya Sekondari iliyopo kata ya Ludete inayojengwa na fedha za SEQUIP kiasi cha shilingi 584,280,029
Halmashauri ya wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Saluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa