Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, amewataka wananchi wa kata ya Nyamboge kushirikiana na serikali kupambana na maneno ya uzushi yanayosambaa katika maeneo mbalimbali. Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Nyamboge, Mhe. Komba alitoa tahadhari juu ya taarifa zisizo na ukweli zinazodai kuwa kuna watu wanang'olewa figo.
“Kuna maneno ya uzushi yanayosema watu wanang'olewa figo, lakini baada ya uchunguzi niliofanya kwa polisi na wananchi, hakuna tukio lolote kama hilo lililoripotiwa. Ni muhimu tuelewe kuwa uzushi huu unaweza kusababisha taharuki na kuleta madhara kwa jamii,” alisema Mhe. Komba.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Abdallah Komba akizungumza na wananchi wa kata ya Nyamboge katika mkutano wa hadhara ulifanyika katika kata hio
Tahadhari Dhidi ya Wizi wa Watoto
Mhe. Komba pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia suala la wizi wa watoto, akieleza kuwa uzushi kama huo unaweza kuwapa fursa watu wenye nia mbaya. Alisema, "Panapokuwa na maneno ya uzushi, watu wenye nia mbaya wanaweza kutumia fursa hiyo kufanikisha matendo yao maovu. Tunapaswa kuongeza nguvu na kushirikiana kama jamii ili kuhakikisha usalama wa watoto wetu."
Alisisitiza umuhimu wa ulinzi shirikishi katika ngazi ya jamii, akiwataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu kama vile wizi, ubakaji, na uporaji, ili kusaidia serikali kudhibiti vitendo hivyo.
Wananchi wa kata ya Nyamboge wakifuatilia kwa makini mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hio Oktoba 24, 2024
Mwenge wa Uhuru 2024
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa mwaka 2024, Mwenge wa Uhuru utapita katika kata ya Nyamboge, ambapo miradi mbalimbali itazinduliwa na wananchi watapata nafasi ya kushiriki. Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge na kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizo.
“Wajibu wetu ni kujitokeza kwa wingi hapa Nyamboge na baadaye kushirikiana kukesha viwanja vya stand ya Nkome,” alihimiza Mhe. Komba.
Ushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Aidha, Mhe. Komba alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa. Alisema, “Jitokezeni kwa wingi kupiga kura ili tupate viongozi bora watakaosaidia kusukuma mbele maendeleo ya kata yetu.”
Utatuzi wa Kero za Maji na Umeme
Katika mkutano huo, wananchi wa kata ya Nyamboge walimweleza Mhe. Komba changamoto za upatikanaji wa maji katika kijiji cha Lukaya, ambapo mradi wa maji unaotumia nishati ya sola umeshindwa kusukuma maji ya kutosha kutokana na nguvu ndogo ya sola hiyo. Aidha, kijiji cha Chilameno kililalamikia kutokuwa na kisima cha maji.
Mwananchi kutoka kata ya Nyamboge akitoa kero ya maji, katika kijiji cha Lukaya mbele ya mkuu wa Wilaya ya Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba (katikati) akizikiliza kero ya mwananchi wa kata ya Nyamboge
Mhe. Komba alieleza kuwa kuna mradi mkubwa wa maji unaoendelea kutekelezwa, ambao utahusisha pia kata ya Nyamboge. Pia aliagiza mamlaka ya maji RUWASA kuhakikisha wanatekeleza mradi wa ujenzi wa kisima katika kijiji cha Chilameno.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Hashim Komba (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa RUWASA Charles Sunday (wa pili kulia) juu ya utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa Nyamboge
Katika suala la umeme, wananchi walilalamikia baadhi ya vijiji kutokufikiwa na nishati hiyo. Mhe. Komba alibainisha kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha umeme unafika kwenye kila kijiji, na kuwa wananchi wanapaswa kuwa na imani kwamba serikali iko kwenye mchakato wa kutatua changamoto hiyo.
Changamoto za Kilimo na Elimu
Mhe. Komba pia alizungumzia changamoto za kilimo, ambapo wananchi walieleza kuwa bei ya pembejeo ni ya juu, hali inayokwamisha maendeleo ya kilimo katika kata hiyo. Mhe. Komba alifafanua kuwa serikali inachukua hatua za kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa bei nafuu ili wakulima waweze kuzimudu.
Aidha, alisisitiza kuwa changamoto za elimu pia zimetatuliwa na serikali kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha sekta hiyo kwa manufaa ya wananchi wote.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dr. Modest, pamoja na wataalamu kutoka halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa