Na Michael Kashinde
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Geita na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga wakizungumza na makarani wa Sensa wanaoendelea kupatiwa mafunzo wamewataka kutanguliza uzalendo katika zoezi wanalokwenda kulisimamia Agosti 23 mwaka huu.
Mhe. Shimo akizungumza na Makarani hao Agosti 3 na 4 katika Shule ya Sekondari Bugando na Shule ya Msingi Nyarugusu ambapo kuna vituo vya kutolea mafunzo kwa Makarani wa Sensa amesema kuwa zoezi hili ni zaidi ya Ukarani kwa kuwa Serikali inawategemea wao kuiwakilisha Nchi na Taifa ili kupata takwimu sahihi.
Amesema kuwa zoezi hilo ni kubwa na litaisaidia Serikali kupanga mipango yake kwa usahihi baada ya kupata takwimu halisi za wananchi wake hivyo amewataka kutumia mbinu mbalimbali wanazofundishwa zitakazowasaidia kupata ushirikiano wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi ili na wao wawe huru kutoa taarifa sahihi zinazohitajika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Wanga ambaye amekuwa na desturi ya kupitia vituo hivyo kila siku tangu mafunzo hayo yameanza amekuwa akitoa wito kwa Makarani hao kutunza vifaa mbalimbali wanavyopewa kwa ajili ya zoezi hilo na kuvitumia kwa kazi iliyopangwa pekee.
Adv. Wanga amesema kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kununua vifa hivyo ili kufanikisha zoezi la Sensa akitolea mfano wa kifaa kinachoitwa Kishikwambi kuwa kinahitaji umakini wa hali ya juu kwa kuwa kuharibika au kupotea kwa kifaa hicho kunaweza kupoteza pia taarifa muhimu suala linaloweza kuharibu zoezi huku akisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa wale watakaojaribu kuharibu zoezi kwa uzembe.
Michael Francis Bundala ambaye pia ni karani wa Sensa mwaka 2022 aliyekuwa akipatiwa mafunzo katika Shule ya Sekondari Bugando baada ya kufanya Mtihani wake Agosti 5 amesema kuwa wanashukuru kwa mafunzo hayo ambayo yamewapa pia majibu ya mitihani hiyo akieleza kuwa mafunzo hayo yana tija hata wakienda kazini watakuwa na uelewa wa kutosha kufanya zoezi hilo.
Makarani wa Sensa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanaendelea kupatiwa mafunzo katika vituo ya Bugando, Nyarugusu na Katoro ikiwa ni sehemu ya maadalizi ya msingi kabisa kuelekea zoezi hilo la kitaifa la kuhesabu watu ambao watalala nchini usiku wa Agosti 23, Kwa kauli mbiu ya "SENSA KWA MAENDELEO, JIANDAE KUHESABIWA'' ni dhahiri kuwa kila mtanzania anawajibika katika kufanikisha zoezi hili hivyo kila mtu kwa nafasi yake akiamua pia kumhamasisha na jirani yake bila shaka litafanikiwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa