MAHAKAMA Kuu Kanda ya Geita leo Januari 28, 2025 imetoa Elimu ya masuala ya sheria kwa watumishi wa umma Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuwajengea uwezo Watendaji wa kata na vijiji katika maeneo yao ya kazi.
Awali akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita –Nzera, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Geita Mhe Kevin Mhina amesema Mahakama Kuu kanda ya Geita imeona umuhimu wa kuwapatia elimu ya maswala ya sheria watendaji kwani ni watu muhimu katika utumishi wa umma kuisaidia jamii.
“Tunatambua umuhimu wa watendaji kwenye mnyororo wa haki na muunganiko wa kazi zenu na kazi za haki na maswala yote yanayohusu mambo ya mahakama katika majukumu yenu kama watendaji katika jamii kwa mustakabali wa nchi na mkoa wetu wa Geita”Amesema Mhe Jaji Mhina.
Mhe Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Geita Kevin Mhina akizungumza na watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera
Aidha Mhe Jaji Mhina amesema kuwa mahakama hiyo inatumia mifumo na hakuna matumizi ya karatasi lengo likiwa ni kuendana na teknolojia ya dunia na kuongeza kuwa mahakama hiyo katika wiki ya sheria imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maswala ya kisheria.
Kwa Upande wake Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Mpatanishi wa Migogoro Nchini, Ndg Majaliwa Yohana amewakumbusha watendaji hao majukumu yao katika jamii hususani katika maswala ya kisheria iliwaweze kuisaidia Halmashauri na kuepusha migogoro katika jamii.
Aidha Majaliwa amewataka watendaji hao kusimamia maswala ya usalama na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao ya utawala ikiwa ni pamoja na kupitia mipango na bajeti pamoja na kusimamia utekelezaji wake sambamba na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Naye Hakimu Mkazi Mahakama ya Geita Mhe Frank Waane amewataka watendaji hao kwenda kusimamia na kutekeleza amri za mahakama, na usuluhishi wa maswala ya ndoa kwani wao wana nafasi katika muhimili wa mahakama.
“Watendaji wa Vijiji na Kata wanatambulika kisheria chini kifungu cha 51 na 56 cha sheria ya mahakimu ya mahakama sura ya 11 ya mwaka 2019 kuwa ni walinzi wa amani katika maeneo wanayo yahudumia. Amesema Mhe Waane.
Katika mafunzo hayo, Mhe Mary Kazungu, msaidizi wa sheria wa Jaji Mahakama kuu kanda ya Geita amewakumbusha watendaji hao majukumu yao mahakamani katika utoaji wa ushahidi kwa kuwa wanapata taarifa mbalimbali juu ya migogoro inayowakabili wananchi katika maeneo yao.
Mhe Mary Kazungu, msaidizi wa sheria wa Jaji Mahakama kuu kanda ya Geita akizungumza na watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera
Mhe Kazungu amewataka watendaji hao kuwaelekeza wananchi mabaraza yanayotoa huduma za usuhishi wa ndoa kwa kuwa yanatambulika kisheria chini ya kifungu cha 102 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na yamewekwa katika ofisi za kata na sio kijiji.
Vilevile watendaji hao wametakiwa kuwafichua wahamiaji haramu katika maeneo yao ya utawala. Hayo yamesemwa na Afisa Uhamiaji Koplo Isihaka Abasi ambapo amewataka watendaji kushirikiana na maafisa uhamiaji kata kwa ajili ya kidhibiti wahamiaji haramu wanaoingia katika maeneo yao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt Modest Burchad ameishukuru Mahakama ya Kanda Mkoa wa Geita kwa kutoa mafunzo kwa Watendeji hao ili kuwajengea uwezo katika maeneo yao ya kiutendaji katika Halmashauri.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Geita Mhe Bruno Fredrick akiwaasa Watendaji wa Kata na Vijiji kuzingatia uandishi wa maungamo kunapolekea kufutwa kwa kesi nyingi kwa kuwa yanakosewa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa