Na: Hendrick Msangi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndugu Karia Rajabu Magaro, amefanya ziara kwenye mradi wa shule ya Sekondari Nyakaduha iliyopo kata ya Isulwabutundwe Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Mkuregenzi huyo kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa za serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ujenzi huo wenye jumla ya madarasa 8 maabara 3, chumba cha kompyuta (ICT room) 1, maktaba 1, matundu 8 ya vyoo na jengo la utawala 1 unatekelezwa na fedha za SEQUIP ambazo ni jumla ya shilingi 584,280,029.
Katika ziara hiyo Magaro alimtaka Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Mvugusi Laurence ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Ujenzi wa shule hiyo kushirikiana na Kamati zote zinazohusiana na mradi huo ili ukamilike mapema kwani muda wa kukamilika kwa mradi huo umeshapita.
” Hakikisheni vifaa vinanunuliwa kwa pamoja sio kununua vifaa nusunusu ambapo kunaongeza gharama za usafirishaji, ili kazi ifanyike kusiwepo sababu ya ukosefu wa vifaa.
Pia malipo yafanyike kwa wakati kwa mzabuni anayeleta vifaa na kwa mafundi ili kuongeza kasi ya kukamilika kwa mradi huu.” alisema Magaro.
Aidha alielekeza idadi ya mafundi kuongezeka kwani ni wachache kulinganisha na kazi iliyopo pamoja na kukaa na kamati ya manunuzi pamoja na mzabuni kufanya kazi kwa pamoja na sio kuweka maslahi mbele ili mradi huo ukamilike mapema.
Ndugu Karia Rajabu Magaro Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akikagua Ujenzi wa Mradi wa Shule ya Sekondari Nyakaduha kata ya Isulwabutundwe.
Mradi huo utakapokamilika utaweza kuchukua jumla ya wanafunzi 205 kutoka shule za msingi za Nyakaduha (95) Mlimani (41) na Igaka (69) Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaishukuru serikali kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya mradi huo ambapo utakapokamilika utawanufaisha wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda kwenye shule nyingine.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa