Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga ameshauri baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwashirikisha watendaji wa kata katika vikao hivyo ili waone uwasilishaji unavyofanyika suala litakalowaongezea ujuzi wa kuandika taarifa za kata zao.
Ametoa ushauri huo leo Novemba 11,2021 akiwa katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo amewataka pia Madiwani hao kuweka taarifa za Mapato ya kata husika sambamba na taarifa za ukatili kwa wanawake na watoto.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mheshimiwa Charles Kazungu amewakumbusha Waheshimiwa Madiwani kuandaa vizuri taarifa zao kwa kuainisha changamoto zote zilizopo kwenye kata zao ili ziweze kutafutiwa utatuzi huku akisisitiza kuwa taarifa hizo zinawasilishwa kwenye mamlaka za juu.
Katika mkutano huo wajumbe ambao ni Waheshimiwa Madiwani wamepata nafasi ya kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata kwa kipindi cha Julai hadi Septemba ,2021.
Aidha mkutano huo wa baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022 unatarajiwa kuendelea tena hapo kesho kwa kujadili taarifa hizo mbalimbali zilizowasilishwa siku ya leo na Madiwani hao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa