Na: Hendrick Msangi
Madiwani kutoka Halmashauri ya wilaya ya Geita leo Novemba 16, 2023 wamepata huduma ya upimaji wa afya na timu ya madakari kutoka hospitali ya Nzera iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Zoezi hilo limeafanyika wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani ukiendelea kwa siku mbili Novemba 15 na 16 ambapo waheshimiwa madiwani walijitokeza kwa ajili ya upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza yenye kauli mbiu “Usijasahau jali Afya yako”
Awali akitoa elimu juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza , Dkt Manigina Filemoni ambaye pia ni mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza Wilayani Geita amesema utafiti unaonyesha magonjwa hayo ambayo ni Kisukari, seli mundu na presha (BP) yamekuwa na athari kubwa sana ambapo asilimia 33 ya vifo vinatokana na magonjwa hayo.
Waheshimiwa Madiwani wakiwa kwenye foleni katika zoezi la upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, zoezi hilo limeambatana na kikao cha baraza la madiwani linalomalizika leo Nevemba 16, 2023.
Aidha Dkt Manigina alisema lengo kuu ni kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uelewa wananchi juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuwataka Madiwani hao kuwa mfano kwa kupima afya zao na kuwasisitiza kuwa makini na mtindo wa maisha ambao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa magonjwa hayo “Usipokula chakula kama dawa utakula dawa kama chakula hivyo ni vema kupima mapema ili kuwahi kugundua tatizo na kuchukua hatua mapema” alisema Dkt Manigina.
“Lengo la juma hili kutoa uelewa na kufanya uhamasishaji wa kufanya vipimo vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kuanza na viongozi ili waeze kuchukua hatua madhubuti kwa kutoa elimu kwa wananchi ili kuinusuru jamii na kupunguza athari za magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Dkt Manigina.
Dkt, Manigina Filemoni ambaye ni mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza Halmashauri ya Wilaya ya Geita akitoa ushauri kwa Mheshimiwa Daudi Mlekwa Diwani kata ya Nyamboge
Wakieleza kuhusu huduma hiyo baadhi ya madiwani akiwepo Mhe Renatus Ndelembi diwani wa kata ya Nyawilimilwa alisema amepima afya na amepokea ushauri wa Madaktari ambapo ataanza kuchukua tahadhari juu ya magonjwa yasiyo yasiyo ya kuambukiza.
“Nimepata ushauri mzuri wa madaktari wamesema nisizidishe chakula kingi cha wanga, uzito wangu upo sawa nipo vizuri nitaendelea kufanya vipimo mara kwa mara” alisema Mhe. Ndelembi.
Naye Diwani wa kata ya Bukondo Mhe Thomas Msongareli ameshauri wananchi ambao hawana desturi ya kupima afya zao wajitokeze kwa wingi ili kujua afya zao kabla athari hazijawa kubwa.
Madiwani hao waliishukuru serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kurahisisha huduma za afya kwa kuendelea kutoa vifaa vya kupima afya ambapo zoezi hilo halina gharama kwa kipindi cha maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kuwajali watu wake kwani ndio rasilimali ya maendeleo ya Taifa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa