Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani mnamo Novemba 25, 2024, katika Kata ya Nyaruyeye, kwa lengo la kuhamasisha jamii kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuhimiza umuhimu wa kujua hali za afya. Tukio hilo lililofanyika chini ya kauli mbiu "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI" lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe khadija Said, akizungumza na wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yaliyofanyika katika Kata ya Nyaruyeye.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mheshimiwa Khadija Said, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamigota, aliongoza maadhimisho hayo na kusisitiza umuhimu wa kila mmoja kujitokeza kwa upimaji wa hiari.
"Afya zetu ndizo msingi wa kila kitu. Kupima afya ni hatua ya kwanza ya kujilinda na kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Niwaombe ndugu zangu, tujitokeze kwa wingi kufuatia maadhimisho haya," alisema Mheshimiwa Khadija.
Wananchi wa Kata ya Nyaruyeye wakiwa katika zoezi la upimaji wa afya, katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi
Maadhimisho hayo yalihusisha huduma za bure za upimaji wa VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza, yakifanikishwa kwa ushirikiano na mashirika kama ICAP, SHDEPHA, HACOCA, na H-PON. Wananchi waliojitokeza walitoa shukrani kwa huduma hizo, wakisisitiza umuhimu wa kuwa na taarifa sahihi kuhusu hali zao za kiafya.
Wananchi wa kata ya Nyaruyeye wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya ukimwi
Ernest Daudi Gawile, mkazi wa Nyaruyeye, alisema:
"Nimepima afya yangu kwa sababu nimeona umuhimu wake, hasa kwa kuwa huduma hizi ni bure. Nawashauri wananchi wenzangu, tusikose nafasi kama hii."
Kwa upande wake, Musa Stephano, mchimbaji wa madini, alisema mazingira ya migodini yamekuwa na changamoto kubwa za maambukizi, hivyo hatua ya kujua hali ya afya ni muhimu sana.
Kwa mujibu wa Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Bi Mathalene Mgina, amesema takwimu za hivi karibuni zinaonesha idadi kubwa Zaidi ya maambukizi kwa wanawake wa umri kati ya miaka 15-24 ukilinganisha na idadi ya wanaume wanaoambukizwa katika umri huo. Aliongeza kuwa idadi kubwa ya maambukizi ipo katika maeneo ya machimbo ya dhahabu na mialo ya uvuvi, ambako hali za kijamii na kiuchumi zinachochea maambukizi.
Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikabidhi msaada wa sare za shule na madaftari kwa watoto 40 wanaoishi na virusi vya ukimwi Pamoja na wanaotoka kwenye mazingira hatarishi ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI., huku akitoa shukrani kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa mchango wao mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Mhe Khadija Said, Mgeni rasmi akikabidhi msaada wa mahitaji ya shule, kama Sare za shule na daftari kwa wanafunzi wenye wanaoishi na Maambukizi ya virusi, misaada hiyo ilipokelewa na waalimu wakuu
"Ni muhimu tushirikiane sote kama jamii na wadau mbalimbali ili kufanikisha jitihada za Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huu," alisisitiza Mheshimiwa Khadija.
Burudani kutoka Kwaya ya Mwanzo Mgumu ya Nyaruyeye iliwapa hamasa washiriki wa tukio hilo, lililoweka alama ya kudumu kwa jamii ya Nyaruyeye kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za kinga, kujua hali za afya, na kuishi kwa tahadhari zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa