Imeelezwa kuwa kutokuunganishwa kwa umeme wa REA hadi sasa katika maeneo mengi ya Wilaya ya Geita, hususani kata za Isulwabutundwe na Vijiji vyake vya Igaka,Ibisabageni na Nyakaduha kumesababishwa na Mkandarasi aliyepewa kazi ya kuunganisha umeme katika Mkoa wa Geita amejitoa.
Bw.Joseph Essau kutoka ofisi za TANESCO Wilaya ya Geita amenukuliwa alipokuwa akijibu maswali ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Novemba 12, 2021 katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2021/2022, uliokuwa ukijadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2021.
Maswali ya msingi ya Mh.Sabina Mathias Lupuga diwani wa viti maalumu na Mh.Renatus Marco Ntelembi diwani wa kata ya Nyawilimilwa walitaka kujua ni lini huduma hiyo itawafikia wananchi wa kata za Isulwabutundwe, Kakubilo na Vitongoji vyote vya Nyawilimilwa na Ntinachi.
Akijibu Maswali hayo Bw.joseph Essau alisema kuwa Mkandarasi aliyepewa kazi ya kuunganisha Mradi wa umeme wa REA katika Mkoa wa Geita alijitoa, ambapo kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na TANESCO wanaendelea kumtafuta mkandarasi mwingine wa kuendelea na kazi hiyo huku akiahidi ndani ya kipindi cha miezi mitatu atakuwa amepatikana.
Aidha bw.Essau amewataka waheshimiwa madiwani kuwaondoa hofu wananchi na kuwataka kuwa subira kwa kipindi hiki cha kusubiri mkandarasi apatikane huku akisisitiza kuwa kazi hiyo itakapoanza itafanyika kwa haraka na kwa umakini mkubwa ili kuwasaiidia wananchi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mh.Renatus Ntelembi diwani wa kata ya Nyawilimilwa umeme haujafika katika kijiji cha Kibwela na umeme Jazirishi unahitajika katika Vitongoji vyote vya Nyawilimilwa na Ntinachi.
Huduma hiyo ya nishati ya umeme inahitajika katika kata ya Isulwabutundwe na vijiji vyake vya Igaka, Ibisabageni, na Nyakaduha na baadhi ya maeneo ya kata ya Kakubilo na vijiji vyake vya Barasana,kabayole,Luhala na Kikwete kama alivyoeleza diwani wa viti maalumu Mh.Sabina Lupuga.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa