Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg Godfrey Eliakimu Mnzava amepongeza namna miradi ya maendeleo inavyotekelezwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Mnzava ameyasema hayo wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Oktoba 5, 2024 wakati ulipokimbizwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita umbali wa 45.6 km kutoka eneo la mapokezi kata ya Bugulula hadi eneo la mkesha kata ya Nkome na Kuzindua, kuona,pamoja na kuweka mawe ya Msingi katika Miradi mbalimbali ya maendeleo.
KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
“Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu” ni kauli mbiu ambayo imetawala kila kona ya Nchi ya Tanzania kufuatia tukio kubwa la Kikatiba na kidemokrasia litakalofanyika Novemba 27, 2024 kote nchini la uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ndg Mnzava amewasihi wananchi kuendea kutunza amani ya nchi kwa wivu mkubwa na kuwataka kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 ikiwa ni pamoja na kuwataka wananchi kuchuja na kuwapima wagombea huku wakiepuka rushwa. “Tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara ya wagombea ili kusikiliza sera zao, uwezo wao na kisha kuchagua viongozi watakaotuunganisha na kutuletea maendeleo” amesema Mnzava.
UWEZESHAJI WA VIJANA KUPITIA MIKOPO YA HALMASHAURI
Mwenge wa Uhuru 2024 umetembelea kikundi cha vijana Masakuro chenye mradi wa kukodisha baiskeli ambacho kilikopeshwa kiasi cha shilingi milioni 15 na Halmashauri kwa ajili ya kuendesha mradi wa kukodisha baiskeli ambapo Ndg Mnzava amekipongeza kikundi hicho cha vijana kwa namna kinavyoendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na kurejesha mkopo huo kwa wakati.
Pamoja na pongezi hizo ndg Mnzava ameitaka Halmashauri kuendelea kuviratibu na kuvisimamia vikundi vingine vinavyopewa mikopo na serikali ili kurejesha kwa uaminifu ili kuendelea kujenga uchumi.
UTEKELEZAJI WA MIRADI KUPITIA MAPATO YA NDANI
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ndg Godfrey Eliakimu Mnzava akiwa kata ya Nzera amezindua ofisi ya Kata iliyojengwa kwa mapato ya ndani jumla ya shilingi 117,257,879.
Mnzava ameipongeza Halmashauri kwa kutenga mapato ya ndani kujenga ofisi kisasa ambayo watumishi watafurahia kufanya kazi katika ofisi hiyo.”Tumefurahishwa kwa namna ambavyo Halmashauri imetenga fedha za mapato ya ndani kujenga ofisi ya kisasa kwa ajili ya watumishi watakaofanya kazi katika mazingira mazuri na ya kupendeza” amesema Mnzava
UIMARISHAJI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika kata ya Nzera umeweza kuweka jiwe la msingi kwenye barabara ya lami nyepesi inayosimamiwa na TARURA yenye urefu wa kilometa 1.1 yenye thamani ya shilingi milioni 737, 494,984.00 ambazo ni fedha zitokanazo na tozo ya mafuta.
Ndg Mnzava ameipongeza TARURA kwa namna wanavyotumia mfumo wa manunuzi NEST katika kutekeleza mradi huo. “Lengo la Serikali ni kuendelea kuboresha maisha ya wananchi, vitendo ni utekelezaji na tumeona hivyo ni wasihi wananchi kuendelea kutunza miradi hii.” Amesema Mnzava.
UTEKELEZAJI WA FALSAFA YA MWENGE WA UHURU
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka maneno ya Kifalsafa kwa kusema “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumani pale ambapo hakuna matumani , ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo jaa dharau.
Hii imedhihirika pale ambapo Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa ndg Mnzava alipogawa Bima ya Afya ya jamii iliyoboreshwa (ICHF), Sukari, Penseli na madaftari kama sehemu ya zawadi kwa watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na familia zao.
Akigawa vifaa hivyo ndg Godfrey Mnzava kwa watoto hao ambao wamewakilisha watoto wengine wenye mahitaji maalumu ambao wako katika maeneo mbali mbali ya Halmashauri ametoa wito kwa jamii kuonyesha upendo kwa watoto hao.“Tusiwanyanyase tuendelee kuonyesha upendo kwa watoto wenye mahitaji maalum”. Amesema Mnzava.
MIRADI YA AFYA
Mwenge wa Uhuru umetembelea na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Kituo cha afya Kata ya Nkome chenye majengo matatu Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Jengo la Maabara, na Wodi ya Wazazi (Maternity) unatekelezwa kupitia Mpango wa CSR huku ukitarajiwa kukamilika tarehe 31 Oktoba 2024 ambapo wananchi wa Nkome wapatao 60,000 hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya.
Kituo hicho kitapunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Nzera.
MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA
Mwenge wa uhuru 2024 umeendelea kuhamasisha kampeni ya kupambana na malaria kupitia kauli mbiu isemayo “Ziro Malaria inaanza na Mimi- Nachukua hatua kuitokomeza” ambapo kiongozi wa mbio za Mwenge ndg Mnzava amegawa vyandarua kwa wawakilishi wa makundi maalumu (wazee, wajawazito na Watoto) ili kujikinga na mbu waenezao Malaria.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita imefanya kampeni ya kitaifa ya ugawaji wa vyandarua kwenye jamii (kaya) kwa kata zote 37 kwa kipindi cha mwezi August hadi Oktoba 2024, ambapo kaya 175,337 (asilimia 95), watu 1,234,473 (asilimia 112) waliandikishwa na jumla ya vyandarua vilitolewa kwa kaya zote ni 660,734. Vyandarua vya kampeni vimetolewa nchini kwa ufadhili wa JHUCCP na USAID kupitia Mfuko wa Rais wa Kudhibiti Malaria (PMI).
MAZINGIRA
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 imeweka masharti yanayozuia uharibifu na uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kusimamia sheria,kanuni na miongozo inayotolewa na serikali juu ya uhifadhi wa Mazingira, misitu na rasilimali zake, Halmashauri ya wilaya ya Geita imeendelea kutambua juhudi na mchango wa wananchi na vikundi vinavyojishughulisha na hifadhi ya mazingira na kuenzi juhudi za wananchi wanaojitolea kutunza, kusimamia na kuhifadhi mazingira ambapo kiongozi wa Mbio za Mwenge amekabidhi vifaa vya usafi kwa kikundi cha usafi cha Red cross kata ya Nkome venye thamani ya shilingi milioni 2. Aidha katika kuyatunza mazingira Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg Godfrey Eliakimu Mnzava ameweka jiwe la Msingi pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu katika shamba la miti lililopo kijiji cha Igate linalomilikiwa na mwananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zikiwepo shule, miradi ya afya, maji na miundombinu mizuri katika kuendelea kukuza uchumi wa Taifa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa