Katika kuendeleza ushirikiano kwenye majukumu mbalimbali ya ujenzi wa Taifa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe.Charles Kazungu amewataka wataalamu kuwashirikisha moja kwa moja Madiwani katika kuandaa taarifa za kata zao.
Ametoa wito huo Februari 2, 2022 wakati akiahirisha mkutano wa kawaida wa baraza la Madiwani wa robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa siku ya kwanza uliokuwa unapokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2021.
Mhe.Kazungu amewataka madiwani kushirikishwa katika uandaaji wa taarifa hizo za kata ili wawe na uelewa wa kutosha kwa kuwa wao ndio wanaoziwasilisha taarifa hizo katika mikutano ya mabaraza huku akiwashauri wataalamu hao kuandaa mchanganuo wa matumizi ya fedha za uviko 19 hali itakayoisaidia Halmashauri kuwa na makisio sahihi ya ujenzi wa miundombinu mingine ya aina hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga ametoa wito kwa Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya kufuatilia changamoto za mgawanyiko wa viongozi hasa wanasiasa katika kata Nyawilimilwa zinazosababisha ushawishi kwa wananchi wasichangie miradi ya maendeleo.
Wito huo umekuja kufuatia taarifa ya kata ya Nyawilimilwa kuonesha changamoto hiyo ya mgawanyiko wa viongozi wa siasa ambao wametofautiana na kushawishi wananchi wasichangie shughuli ya maendeleo ambapo Mkurugenzi Wanga amekemea hilo na kutoa wito wa kuwashirikisha wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo ili wawe na uchungu na kile walichokianzisha kwa faida yao.
Baada ya jukumu la siku ya kwanza la kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya kata kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2021 mkutano huo wa baraza la Madiwani unatarajiwa kuendelea tena hapo kesho Februari 3, 2022 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera kwa kujadili taarifa hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa