Mashindano ya Michezo ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) yaliyoanza kutimua Vumbi Agosti 15 Jijini Tanga yamezinduliwa rasmi leo Agosti 23,2025.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mashindano hayo katika viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga, Mgeni Rasmi Naibu Waziri ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Zainab Katimba (MB) amesema michezo ya watumishi wa umma mamlaka za Serikali za Mitaa ni Fursa kwa Halmashauri kuendelea kujitangaza kwa wananchi na kuwafanya watambue zilipo ikiwa ni Pamoja na kuwafahamu watumishi wa Halmashauri hizo kupitia ushiriki wao katika michezo mbalimbali.
Naibu Waziri ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Zainab Katimba (MB) akihutubia viongozi wa ngazi mbalimbali za Halmashauri na wanamichezo katika ufunguzi wa Mashindano ya SHIMISEMITA uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vilevile Mhe Katimba amesema Watumishi wa umma wote walipo katika Halmashauri zote nchini ni chachu ya Maendeleo ya Taifa kwani ndio wanaosimamia utekelezaji wa mipango inayo andaliwa na Serikali Pamoja na utekelezaji wa maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi.
“Watumishi wa umma wanatakiwa kuwa imara kiafya na kiakili hivyo kupitia michezo watumishi wa umma wanapaswa kushiriki kikamilifu ili kuwa na afya njema yenye kuleta ukakamavu, weledi, umoja,upendo, ushirikiano , mshikamano , uaminifu, uzalendo na mahusiano mazuri kazini na ushirikiano wa pamoja na wananchi.” Amesema Mhe Katimba.
Pamoja na hayo Mhe Zainab Katimba, amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuchukua juhudi za Maksudi kuimarisha utamaduni wa Mtanzania na kuimarisha Michezo mahala pa kazi.
Watumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanaoshiriki mashindano ya SHIMISEMITA jijini Tanga, wakipita mbele ya mgeni rasmi, katika ufunguzi wa mashindano hayo jijini Tanga
“Ili kutimiza adhma hiyo nina waagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Majiji na Manispaa kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao katika kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa na kuhakikisha kinapewa fedha za mgao kila mwezi kama divisheni nyingine zilizopo Halmashauri kuwawezesha watumishi wote walio chini ya mamlaka zao kushiriki michezo inayo andaliwa na Shirikisho la Michezo Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania “
Akihitimisha hotuba yake, Naibu Waziri-OR-TAMISEMI, Mhe Katimba amewataka washiriki katika Mashindano hayo ambayo ni ya 40 yaliyozishirikisha jumla ya Halmashauri 150 kati ya Halmashauri 184 kuitumia kauli mbiu ya mashindano hayo kutekeleza kwa vitendo kwa kuonesha mfano ikiwa ni Pamoja na kuwahabarisha wananchi kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025.
Naibu Waziri ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Zainab Katimba (MB), akiwa na viongozi wa jiji la Tanga, wakipunga mkono kwa mamia ya wachezaji wanaoshiriki mashindano ya SHIMISEMITA 2025 jijini Tanga.
“Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuinua sekta ya michezo, Sanaa na utamaduni kuanzia ngazi ya chini ya kitongoji hadi Taifa.” Ameongeza Mhe Katimba.
Mashindano hayo yanaendelea katika viwanja mbalimbali jijni Tanga ambapo Zaidi ya Watumishi 3504 kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa wanashiriki katika michezo na Sanaa za maonesho mbalimbali. Mashindano ya SHIMISEMITA 2025, yamebebwa na Kauli isemayo," Jitokeze kupiga kura kwa Maendeleo ya Michezo”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni Miongoni mwa Halmashauri zilizoshiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Agosti 29, 2025 ambapo jumla ya wanamichezo 63 ikiwa ni Pamoja na Viongozi wa timu na walimu wa timu hiyo wanashiriki Mashindano hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa