Timu za watumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita zimeibuka gumzo jijini Tanga baada ya kufanya vizuri katika Michezo ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) 2025.
Katika mashindano hayo yaliyodumu kwa takribani wiki mbili kwenye viwanja mbalimbali vya jiji la Tanga, timu kutoka Geita zilionesha ushindani mkubwa katika michezo ya mpira wa miguu, pete, wavu na mikono, na kuibua changamoto kwa timu nyingine kutoka halmashauri mbalimbali nchini.
Timu za Mpira wa pete na Mpira wa miguu zikiwa katika michuano ya SHIMISEMITA jijini Tanga
Katika mchezo wa mpira wa miguu (wanaume), timu ya Geita ilishika nafasi ya pili baada ya kutoka sare ya magoli 2–2 dhidi ya Msalala DC, ambayo hatimaye iliibuka mshindi kupitia mikwaju ya penati. Aidha, katika mpira wa mikono (wanaume) Geita ilishika nafasi ya tatu, huku timu ya wanawake ikimaliza nafasi ya nne.
Akizungumza mara baada ya mashindano hayo, Mwenyekiti wa Timu, Mwl. Raphael Ngeleja, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Magaro, kwa ushirikiano mkubwa alioutoa tangu mwanzo wa kambi hadi kufikia tamati ya mashindano. Pia aliishukuru menejimenti ya timu pamoja na wachezaji wote kwa mshikaman o na jitihada walizoonesha, ambazo zimewezesha mafanikio hayo kupatikana.
Timu za Mpira wa wavu na Mpira wa mikono zikiwa katika michuano katika mashindano ya SHIMISEMITA jijini Tanga.
Mashindano ya SHIMISEMITA 2025 yalianza Agosti 15 na yalizinduliwa rasmi Agosti 23 na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga. Mashindano hayo yalifungwa rasmi leo, Agosti 29, na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani.
Uongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wamewatakia pongezi nyingi wachezaji na benchi la ufundi kwa kupandisha juu bendera ya Halmashauri katika mashindano haya, yaliyobeba kauli mbiu: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Watumishi walioshiriki mashindano ya SHIMISEMITA kwa mwaka 2025 wakiwa katika picha ya pamoja.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa