Jamii imeshauriwa kutopenda kuweka taarifa binafsi katika mitandao ya kijamii ili kuepuka kutapeliwa au kuwa watumwa wa baadhi ya watu wenye nia mbaya ambao wanaweza kutumia taarifa hizo kufanya mambo yasiyokubalika katika jamii ikiwemo utapeli.
Rai hiyo imetolewa Septemba 28,2021 na Mhandisi Kadaya Baluhye kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakati wa mafunzo ya matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA) katika Shule za Sekondari Katoro na Mkono Vision, katika mwendelezo wa mafunzo ya matumizi sahihi ya TEHAMA yanayotolewa na Timu ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya TEHAMA Wilaya ya Geita katika maadhimisho ya wiki ya TEHEMA ki Wilaya.
Mhandisi Baluhye amesema kuwa si vyema kuweka taarifa binafsi katika mitandao ya kijamii kwa kuwa uzoefu unaonyesha baadhi ya matapeli wanaweza kutumia taarifa hizo kuwalaghai watu wengine ambao wasipokuwa makini wanaweza kufikiri ni mhusika mwenyewe hali inayopelekea watu kutapeliwa.
Aidha akiongea na wanafunzi wa shule hizo amewaasa kuacha tabia ya kupenda kupiga picha za faragha hasa wasichana pindi watakapokuwa na umri wa kuanzisha mahusiano, kwa kuwa wakati mwingine baadhi ya watu hasa wanaume wanatumia picha hizo kutaka fedha kwa kutishia kuzisambaza suala linalowageuza kuwa mateka wa watu kwa kuhofia fedheha.
Akiwasilisha mada ya Maktaba Mtandao Bw.Frank Makonda Mkuu wa Idara ya TEHAMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita amesema kuwa, matumizi ya TEHAMA kwa Mwanafunzi ni kwa ajili ya kujisomea pekee huku akiwahamasisha kutumia huduma rahisi ya maktaba mtandao Kwa lengo la kuongeza maarifa na sio kwa mambo yasiyowasaidia kitaaluma.
Kwa upande wake Bw.Thomas Novatus Festus Mkuu wa Idara ya TEHAMA katika Halmashauri ya Geita mji akiwasilisha mada ya faida za matumizi ya TEHAMA, amesema kuwa TEHAMA ina faida nyingi kwa mwanafunzi kama vile kufanya tafiti,kujisomea kwa mtandao na hata kuomba mikopo ya elimu za juu huku akisema kuwa Serikali ina mpango wa kuleta vifa vya TEHAMA mashuleni ili kukuza taaluma hiyo.
Aidha Bi.Mwanne Abdallah Afisa usajili wa vizazi na vifo kutoka RITA akizungumza pia na wanafunzi hao amesema kuwa TEHAMA inasaidia sana katika kutunza taarifa za mteja huku akisisitiza kuwa kuna huduma ya usajili kwa njia ya mfumo suala linaloweza kufanywa bila ya kufika sehemu husika kufuatilia cheti cha kuzaliwa huku akiwahamasisha wanafunzi hao kuingia kwenye mfumo kufuatilia vyeti vyao vya kuzaliwa.
Semina hiyo ni mwendelezo wa kuwafikia wadau mbalimbali na kuwaelimisha matumizi sahihi ya TEHAMA katika kuadhimisha wiki ya TEHAMA Wilayani Geita, ikiwa ni Utekelezaji wa kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inayosema ‘’TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu itumie kwa usahihi na uwajibikaji’’suala linalowataka wadau wote wa TEHAMA zikiwemo taasisi zilizopewa dhamana hiyo kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa