Kamati ya siasa ya Wilaya ya Geita, ikiongozwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, Komredi Michael Msuya, kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Komredi Barnabas Mapande, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Abdallah Komba, na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dr. Modest B. Lwakahemula, imekagua njia ya Mwenge wa Uhuru kwa kupitia miradi inayotarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ndani ya Halmashauri ya Geita Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Kamati hiyo iliambatana na wajumbe wake, wakiwemo Komredi Aisha Juma, Komredi Titus Kaguo, Komredi Joyce Omingo, na Komredi Pauline Majogoro, pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Kamati ya siasa ikiongozwa na komredi Msuya (wa nne kutoka kushoto) ikipokea ripoti ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na matundu nane ya Choo katika shule ya sekondari Kasota.
Kamati ilianza kwa kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na matundu nane ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kasota. Mkuu wa Wilaya, Mhe. Komba, alibainisha kuwa halmashauri hiyo inatoa mfano bora wa namna serikali inavyoendelea kuboresha huduma za elimu. Alisema, "Halmashauri hii ina jumla ya shule 77, ambapo 74 ni za serikali. Katika kipindi cha Januari hadi Juni, jumla ya madarasa 90 na matundu ya vyoo 144 yamejengwa. Hii ni jitihada kubwa inayofadhiliwa na serikali, ikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia."
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba (kushoto) akielezea mafaniko ya mradi katika shule ya sekondari kasota, kulia ni Komredi Michael Msuya katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya
Mwonekano wa nje wa vyumba sita vya madarasa na mwonekano wa ndani katika shule ya Sekondari ya Kasota
Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Komredi Msuya, aliongeza kuwa kamati inaridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, huku akishauri kuboresha mazingira ya shule kwa kuweka mfumo wa uvunaji maji kwa kutumia mabati ya madarasa. Alisema, "Tunapovuna maji na kuimarisha mazingira ya shule, tunawaweka wanafunzi katika mazingira bora ya kujifunzia na hivyo kuongeza ufaulu."
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba (kulia), Komredi Michael Msuya (katikati) Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dr. Modest Lwakahemula wakielekea kukagua matundu ya Choo katika Shule ya Sekondari Kasota
Kamati ya Siasa ikiongozwa na Komredi Msuya ikikagua ujenzi wa matundu ya choo katika shule ya Sekondari Kasota
Kamati pia ilitembelea ujenzi wa barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.1 katika Kata ya Nzera. Walitoa ushauri kwa Mkuu wa Wilaya na watendaji wa halmashauri kuhakikisha ubora wa barabara hiyo ili kuepuka mashimo ya mara kwa mara na kuhakikisha mifumo ya maji inafanya kazi ipasavyo. Mhandisi Cuthbert Robert kutoka TARURA alisema, "Kukamilika kwa barabara hii kutarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuongeza thamani ya ardhi, na kuboresha mandhari ya makazi ya wananchi."
Kamati ya siasa Wilaya ikipokea maelezo ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami nyepesi kutoka kwa mhandisi kutoka TARURA Cuthbert Robert (wa kwanza kulia)
Mwonekano wa Barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.1
Katika kata ya Katoma, kamati ilikagua ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 225,000. Komredi Pauline Majogoro alisifu jitihada za serikali na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Meneja wa RUWASA Wilaya ya Geita, Charles Batakanwa, alisema mradi huo utawanufaisha zaidi ya wananchi 11,009 wa Kata ya Katoma na kuondoa magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim komba (wa pili kushoto) akitoa malekezo ya mradi wa maji uliopo katika kata ya Katoma kwa kamati ya siasa ya wilaya,
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Geita, Charles Batakanwa ( katikati) akielezea jambo kwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Komba (kulia) na katibu mkuu wa CCM wilaya ya Geita Michael Msuya (kushoto) wakiwa juu ya tanki la maji Katoma.
Mwonekano wa Tanki la maji katika kata ya katoma.
Kamati ya siasa ya Wilaya ya Geita imepongeza hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa shukrani kwa serikali kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya wananchi. Miradi yote iliyokaguliwa ipo katika hatua za mwisho za kukamilika na inatarajiwa kuanza kutumika muda mfupi ujao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa