Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiongozwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Elisha Lupuga, pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Fatuma Sisay, madiwani, na wataalamu wa halmashauri hiyo, wamefanya ziara ya kukagua miradi muhimu ya maendeleo katika kata za Nyamigota, Ludete, na Katoro.
Kamati ilianza ziara yake katika kata ya Nyamigota, ambako inatekelezwa mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya AMALI Chibingo kwa gharama ya Tsh 584,280,029. Mradi huo umefikia hatua ya asilimia 40 na unalenga kutoa elimu ya ujasiriamali, biashara, michezo, ufundi, ubunifu, na vipaji kwa wanafunzi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nyamigota na msimamizi wa mradi, Mwl. Renatus M. Martine, alieleza kuwa walimu watatu tayari wamepokelewa kwa maandalizi ya kuanza kufundisha pindi shule itakapokamilika. Pamoja na changamoto za ardhi kutitia na masuala ya manunuzi, kamati ilitoa pongezi kwa hatua zilizofikiwa na kuhimiza suluhisho la changamoto hizo.
Kamati ilitembelea miradi kadhaa katika kata ya Ludete, ikiwemo upanuzi wa Shule ya Sekondari Kagega kwa kidato cha tano na sita unaogharimu Tsh 481,000,000. Wajumbe walihimiza ushirikishwaji wa kamati zote zinazohusika katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha uwazi na kasi inayotakiwa.
Pia, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Msingi Bwawani, unaogharimu Tsh 351,500,000, ulipongezwa kwa maendeleo mazuri. Mradi huu unatarajiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kutoka shule za jirani na kutoa fursa kwa watoto wa maeneo ya mbali kuandikishwa.
Aidha, kamati ilikagua upanuzi wa Shule ya Sekondari Lutozo kwa kidato cha tano na sita unaogharimu Tsh 381,000,000. Kamati ilihimiza kuongeza kasi ya utekelezaji na kuzingatia upanuzi wa nyumba za walimu ili kuboresha mazingira ya kufundishia.
Ziara hiyo ilihitimishwa katika kata ya Katoro, ambako kamati ilikagua ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari unaotarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 17 Februari. Mhe. Faraj Seif, Diwani wa Kata ya Bukoli, aliipongeza timu ya usimamizi kwa hatua nzuri zilizofikiwa.
Kamati ilisisitiza ulipaji wa fedha kwa wakati kwa wakandarasi ili miradi hiyo ikamilike ndani ya muda uliopangwa. Aidha, wajumbe waliwahimiza viongozi kushirikiana na wananchi kwa kuwapa taarifa za maendeleo ya miradi hiyo ili kuongeza uwazi na ushirikiano wa jamii.
Miradi hii, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, upanuzi wa shule za sekondari, na kuboresha miundombinu ya shule za msingi, inalenga kuboresha upatikanaji wa elimu na kupunguza changamoto za msongamano wa wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa