Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Hadija S. Joseph, ikishirikiana na wataalamu wa Halmashauri, imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika majimbo ya Busanda na Geita Oktoba 24, 2024.
Jimbo la Busanda
Katika Jimbo la Busanda, Kamati ilitembelea miradi kadhaa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Amali Chibingo inayolenga kufundisha ufundi, ujasiriamali, na kukuza vipaji. Mradi huo, unaotarajiwa kujengwa miundombinu kumi na moja, ikiwemo maabara, ofisi za utawala, madarasa manne, na vyoo, utahudumia zaidi ya wanafunzi 320 baada ya kukamilika kwa madarasa nane. Mwalimu Leonatus Martin, Mkuu wa Sekondari ya Nyamigota, alitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, ambapo ujenzi uko katika hatua ya kuchimba msingi na kusambaza vifaa vya awali.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamigota Mwl Leonatus Martin akisoma taarifa ya mradi, mbele ya kamati ya fedha ilipotembelea mradi huo
Shughuli mbalimbali za ujenzi zikiendedelea katika eneo la ujenzi wa Shule ya Amali.
Kamati pia ilitembelea mradi wa upanuzi wa Shule ya Sekondari Kagega kwa ajili ya kidato cha tano na sita. Upanuzi huu unahusisha ujenzi wa mabweni mawili, madarasa, na matundu ya choo, ambapo kazi inaendelea kwa kuchimba msingi.
Hatua za awali za uchimbaji wa msingi na kusombelea mahitaji ya ujenzi katika shule ya skkondari Kagega
Aidha, Kamati ilipongeza maendeleo ya mradi wa shule mpya ya msingi inayosimamiwa na Shule ya Bwawani. Ujenzi umefika hatua ya msingi na tayari imetandaza jamvi. Wajumbe walisisitiza umuhimu wa kumaliza miradi kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya elimu katika eneo hilo.
Kamati katika jimbo la Busanda ilimaliza kwa kutembelea upanuzi wa kidato cha tano na cha sita katika shule ya Sekondari Lutozo, ambapo hatua ya msingi na kuweka jamvi imekamilika.
Jimbo la Geita
Katika Jimbo la Geita, Kamati ya Fedha imetembelea Kata ya Usulwabutundwe, ambapo imekagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi (pacha) katika Shule ya Sekondari Nyakaduha, mradi wenye thamani ya Shilingi milioni 100,000,000 chanzo cha fedha kikiwa ni mfuko SEQUP. Kamati hiyo imetoa maagizo kwa fundi anayetekeleza mradi huo kuongeza nguvu kazi ili ujenzi huo ukamilike ifikapo Novemba 30, 2024, sambamba na kuleta vifaa vya ujenzi kwa wakati ili kasi ya ujenzi isisimame.
Ujenzi wa Nyumba ya Mtumishi 2/1 shule ya sekondari Nyakaduha wenye thamani ya shilingi Milioni100,000,000 fedha kutoka mfuko wa SEQUIP. Mradi huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya awamu ya sita kuendelea kuboresha mazingira mazuri katika sekta ya elimu.
Aidha, Kamati imekagua mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Kakubilo wenye thamani ya Shilingi 584,280,029, fedha za SEQUP. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Maeda, ametoa maelekezo kwa mzabuni anayesambaza vifaa vya ujenzi katika mradi huo kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinawasilishwa kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji katika mradi huo.
Kamati ya Fedha uongozi na Mipango pamoja na wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakikagua ujenzi wa Mradi wa Shule mpya ya Sekondari Kakubilo wenye thamani ya Shilingi Milioni 584,280,029 fedha kutoka mfuko wa SEQUIP ambapo kamati imeshauri kila fundi apewe mkataba wa kisheria katika kutekeleza mradi huo ili uweze kukamilika ifikapo Novemba 30, 2024 kama ambavyo mkataba wa ujenzi unavyo elekeza.
Katika ziara hiyo, Kamati ilitembelea pia mradi wa shule mpya ya msingi katika Kata ya Kakubilo, ambao una thamani ya Shilingi milioni 351.500,000, fedha za BOOST. Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ikigijo, Mwalimu Leonsio Mpandachombo Lukas, ambaye anasimamia ujenzi wa mradi huo, amesema kasi ya mradi huo si nzuri kutokana na mzabuni kushindwa kufikisha vifaa kwa wakati na kufanya mafundi ujenzi kushindwa kuendelea na kazi.
Ujenzi wa shule mpya ya Msingi Ikigijo wenye thamani ya shilingi Milioni 351,500,000 fedha kutoka mfuko wa BOOST. Ujenzi wa shule hiyo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi ambapo unatarajiwa kuwa na madarasa 7 ya elimu ya msingi na madarasa 2 ya elimu ya awali na jengo la utawala.
Kufuatia changamoto mbalimbali katika ukamilishaji wa miradi hiyo, Kamati ya Fedha uongozi na Mipango imeitaka Halmashauri kusimamia mikataba ya mafundi ili wakamilishe miradi kwa wakati sambamba na kuendelea kuwashauri wazabuni wengine wenye uwezo kujiunga na mfumo wa manunuzi NEST.
Ukamilishaji wa miradi ya shule hizo unaenda kupunguza msongamano wa Wanafunzi. Hizi ni jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutoa Fedha nyingi kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa